Gavana Tutuba afanya mazungumzo na RC Sawala,viongozi wa Mkoa wa Mtwara

MTWARA-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, amekutana na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala, pamoja na viongozi wengine wa mkoa kujadili maendeleo ya kiuchumi na fursa za uwekezaji zilizopo mkoani humo.
Katika kikao hicho kilichofanyika tarehe 18 Septemba 2025, Gavana Tutuba alisema kuwa uchumi wa Tanzania unaendelea kufanya vizuri kutokana na usimamizi madhubuti wa sera za fedha.

Alibainisha kuwa, Benki Kuu itaendelea kuisimamia kikamilifu sekta ya fedha ili iwe chachu ya ukuaji wa uchumi na kufanikisha Dira ya Taifa ya 2050, inayolenga kufikia uchumi wa Dola trilioni 1 kutoka Dola bilioni 85 za sasa.

Aidha, Gavana alihimiza wananchi kushiriki zaidi katika sekta za uzalishaji kama kilimo, uvuvi, ufugaji wa mifugo na nyuki, huku akiwahamasisha wakulima kutumia Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) ili kunufaika zaidi na mazao yao.

Vilevile, Gavana Tutuba alisisitiza pia umuhimu wa miradi ya maendeleo kutekelezwa kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).

Alibainisha kuwa majadiliano ya mradi mkubwa wa gesi asilia (LNG) yanatarajiwa kukamilika mapema mwaka ujao, mradi ambao utachochea ukuaji wa uchumi wa Mtwara na taifa kwa ujumla.
Katika ajenda ya elimu ya fedha, Gavana Tutuba alisema kuwa BoT tayari imeandaa mitaala na ipo tayari kushirikiana na mkoa wa Mtwara ili kuimarisha uelewa wa wananchi na watumishi wa umma katika masuala ya kifedha.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala, alimpongeza Gavana Tutuba kwa mchango mkubwa wa Benki Kuu katika kuimarisha uchumi wa taifa. Alieleza kuwa zaidi ya asilimia 85 ya uchumi wa mkoa huo unatokana na kilimo cha korosho, mbaazi, ufuta, choroko na mazao mengine.

Mkuu wa Mkoa pia alieleza hatua kubwa zilizopatikana katika sekta za miundombinu, ikiwemo upanuzi wa bandari yenye uwezo wa kuhudumia tani milioni 2 kwa mwaka, uboreshaji wa uwanja wa ndege kwa kuweka taa za usiku, pamoja na ujenzi wa barabara zinazounganisha wilaya za mkoa huo.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na uongozi wa Tawi la Benki Kuu la Mtwara likiongozwa na Mkurugenzi wa Tawi, Bw. Nassor Nassor.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news