DAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Benki ya Maendeleo TIB ulioongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Bw. Sosthenes Kewe. Kikao hicho kimefanyika tarehe 9 Septemba 2025 katika ofisi ndogo ya Makao Makuu ya Benki Kuu jijini Dar es Salaam.
Lengo la ziara ya ujumbe huo ulikuwa ni kumtambulisha Mkurugenzi Mtendaji mpya, Bw. Deogratius Kwiyukwa na kujadili mikakati waliyonayo ya kuimarisha benki hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Gavana Tutuba ameitaka TIB kuzidi kujiimarisha ili kuongeza mchango wake kwenye uwekezaji katika sekta za uzalishaji nchini hasa kwenye viwanda vya kuongeza thamani kwenye maeneo ambayo malighafi za kilimo, mifugo na uvuvi zinapatikana.
Kwa upande wake, Bw. Kewe ameipongeza Benki Kuu kwa usimamizi thabiti wa sekta ya fedha na ameahidi kuwa TIB itaendelea kushirikiana na Benki Kuu pamoja na wadau wengine wa sekta ya fedha kwa ajili ya kustawisha sekta hiyo.


