ZANZIBAR-Mgombea wa nafasi ya Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka Wazanzibari kuepuka siasa za kikanda, kidini, ubaguzi na mifarakano, akisisitiza kuwa mshikamano na amani ni nguzo kuu za maendeleo.
Akizungumza leo Septemba 24,2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika Makombeni, Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, Dkt. Mwinyi amesema,CCM itaendelea kudumisha amani, maridhiano na mshikamano ili Serikali iendelee kutekeleza mipango ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi wote.Ameeleza kuwa, kasi ya maendeleo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita itaongezeka zaidi kupitia miradi mikubwa ya maendeleo.
👉 Sekta ya Afya: Serikali itahakikisha hospitali zote nchini zinatoa huduma za kibingwa, ikiwemo Hospitali ya Abdalla Mzee kupatiwa mashine ya MRI.
👉 Miundombinu: Ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba na barabara ya Chakechake–Mkoani utaiwezesha Pemba kufunguka kiuchumi.
👉 Ajira kwa Vijana: Ajira zitakuwa kipaumbele cha kwanza, Serikali ikihakikisha vijana wengi zaidi wanapata nafasi za kazi.
👉 Zao la Karafuu: Serikali itaendelea kulipa kipaumbele kama zao kuu la uchumi na kuliongezea thamani.



















