Luhaga Mpina aondolewa katika orodha ya wagombea urais, pingamizi lake dhidi ya Dkt.Samia lakataliwa na tume

NA DIRAMAKINI

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imemuondoa Luhaga Joelson Mpina mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha ACT–Wazalendo kwenye orodha ya wagombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Mgombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT - WAZALENDO), Mhe. Luhaga Joelson Mpina akiwa na Mgombea Mwenza, Mhe. Fatma Abdulhabib Ferej. 

Ni kufuatia pingamizi liliowasilishwa na Hamza Saidi Johari, Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya uteuzi wa Luhaga Joelson Mpina kuwa mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo.

Kufuatia kikao chake kilichofanyika tarehe 15 Septemba, 2025 INEC imefanya uamuzi wa kumuondoa Mpina, hivyo kuwa pingamizi pekee lililokubaliwa kati ya mapingamizi manne yaliyowasilishwa mbele yake, ambapo mapingamizi matatu yamekataliwa.

Tume ilipokea mapingamizi matatu tarehe 13 Septemba, 2025 dhidi ya uteuzi wa ndugu Luhaga Joelson Mpina mgombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha ACT – Wazalendo na tarehe 14 Septemba, 2025, ikapokea pingamizi moja dhidi ya uteuzi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan mgombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).

INEC imekataa mapingamizi yaliyowasilishwa na ndugu Almas Hassan Kisabya mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha NRA dhidi ya Luhaga, na pingamizi la ndugu Almas Hassan Kisabya mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha NRA dhidi ya uteuzi wa ndugu Luhaga Joelson Mpina kuwa mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo.

Pingamizi liliowekwa na ndugu Kunje Ngombare Mwilu, mgombea kiti cha Rais kupitia chama cha AAFP dhidi ya ndugu Luhaga Joelson Mpina, mgombea wa Kiti cha Rais kupitia Chama cha ACT Wazalendo limekataliwa pia huku tume ikikataa na kutupilia mbali pingamizi liliowekwa na Luhaga Mpina dhidi ya uteuzi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).



Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news