NA GODFREY NNKO
KATIKA kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa umeendelea kuimarika na kukua kutoka asilimia 6.8 mwaka 2020 na kufikia asilimia 10.1 mwaka 2024.
Aidha, kasi ya ukuaji wa sekta ya madini imeongezeka kutoka asilimia 7.3 mwaka 2020 na kufikia asilimia 8.3 mwaka 2024.
Katika kipindi hicho, Serikali imeendelea kuboresha sheria, kanuni na miundombinu mbalimbali ikiwemo nishati na maji migodini hali ambayo imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kuongeza ufanisi wa kazi katika shughuli za madini.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Fedha na Wizara ya Madini, mafanikio mengine yaliyopatikana ni kuongeza ukusanyaji wa maduhuli kutoka shilingi bilioni 587.3 mwaka 2020/21 hadi shilingi bilioni 875.6 kwa kipindi cha Julai, 2024 hadi Aprili, 2025.
Vilevile, kudhibiti utoroshwaji wa madini, kuhamasisha uwekezaji kwenye shughuli za madini, kurejesha minada ya madini ya vito na ununuzi wa mitambo zaidi ya 10 ya uchorongaji miamba kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
Aidha, Serikali imewezesha upatikanaji wa dhahabu kwa ajili ya Hazina ya Taifa ya fedha za kigeni (Foreign Reserves), ambapo Mpango wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wa Ununuzi wa Dhahabu ulioanza Oktoba 1,2024 umeendelea, kwa dhahabu iliyozalishwa na kuchakatwa hapa nchini.
Mpango huu umeleta mafanikio makubwa katika kuongeza hifadhi ya fedha za kigeni na kuimarisha thamani ya Shilingi ya Tanzania.
Kwa mujibu wa BoT, hadi kufikia Agosti 2025, jumla ya tani 9.165 za dhahabu zenye thamani ya takribani Dola za Marekani milioni 1,015.98 zimeanunuliwa.
Pia, mpango huo umefungua fursa kwa wachimbaji na wauzaji wa dhahabu nchini kuuza dhahabu zao moja kwa moja kwa Benki Kuu ya Tanzania kwa bei ya ushindani kulingana na soko la kimataifa.
Hii inatoa taswira nzuri ya kuongezeka kwa uwezo wetu kama Taifa katika kuongeza thamani kwenye mazao ya maliasili zetu.
Kutokana na mafanikio hayo makubwa katika Sekta ya Madini ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan,hivi karibuni ujumbe maalum kutoka nchini Malawi umewasili nchini Tanzania kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ya usimamizi wa rasilimali madini.
Ujumbe huo, umeongozwa na Mtendaji Mkuu wa Maendeleo ya Biashara ya Vikundi, Zizwan Khonje akiwa ameongozana na wadau wa Sekta ya Madini akiwemo Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Malawi, Percy Maleta na maafisa mbalimbali wa mabenki wa nchini humo na kupokelewa rasmi katika ofisi za mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Dhamira yao wameeleza ni kujifunza kutoka Tanzania kutokana na mafanikio makubwa iliyoyapata katika kusimamia sekta ya madini kwa uwazi, tija na mchango wake katika uchumi wa Taifa.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Katibu Tawala wa mkoa huo, Dkt. Khatibu Kazungu wakati wa kuupokea ujumbe huo amewapongeza wageni hao kwa kuichagua Tanzania kama kituo cha maarifa na uzoefu katika sekta ya madini.
Dkt.Kazungu amesisitiza kuwa, hatua hiyo ni ishara ya kutambua jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuleta mageuzi katika sekta hiyo muhimu.
“Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma na Serikali ya Tanzania, nawakaribisha kwa moyo mkunjufu. Uamuzi wenu wa kuja kujifunza kwetu ni ushahidi wa wazi kuwa tunapiga hatua kubwa katika usimamizi bora wa rasilimali zetu, hasa madini. Hili ni jambo la kujivunia kama taifa,” amesema Dkt. Kazungu.
Dkt. Kazungu ameeleza kuwa, Tanzania kupitia Wizara ya Madini na taasisi zake imefanikiwa kujenga mifumo imara ya usimamizi wa shughuli za utafutaji, uchimbaji, biashara, na usafirishaji wa madini, huku ikizingatia kanuni za uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi katika maeneo yanayozungukwa na shughuli za madini.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Maendeleo ya Biashara ya Vikundi, Zizwan Khonje kutoka Malawi ameonesha kufurahishwa na mapokezi mazuri waliyopewa, na kusisitiza kuwa Tanzania ni mfano wa kuigwa katika Afrika kwa kuwa na sera na mifumo ya usimamizi wa madini inayojali maslahi ya taifa na wananchi.
Khonje amesema, lengo la ziara hiyo ni kujifunza namna ambavyo Wizara ya Madini ya Tanzania imefanikiwa katika usimamizi na urasimishaji wa wachimbaji wadogo, uendeshaji wa masoko ya madini na viwanda vya uongezaji thamani madini.
Ameongeza kuwa, wakiwa nchini ujumbe huo utatembelea maeneo mbalimbali yanayohusiana na uchimbaji, uchenjuaji usafishaji na biashara ya madini ambapo kwa jiji la Dodoma ujumbe huo umetembelea kiwanda cha kusafisha madini ya dhahabu cha Eyes of Africa kwa lengo la kujifunza kwa vitendo mbinu na mifumo inayotumika.
Awali, ujumbe huo ulitembelea ofisi za Wizara ya Madini Mtumba jijini Dodoma ambapo walipata fursa ya kupitishwa kuhusu Sera, Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali inayotumika katika usimamizi wa Sekta ya Madini pia, walipitishwa kuhusu uongezaji thamani madini, usimamizi wa leseni, biashara na masoko ya madini.
Mbali na hayo,ujumbe huo maalum kutoka Serikali ya Malawi umeonesha kushangazwa na kuvutiwa na kiwango kikubwa cha uwekezaji uliofanywa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) katika sekta ya uchimbaji wa madini ya dhahabu mkoani Geita.
Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo ya Biashara za Vikundi nchini Malawi, Zizwan Khonje amesema kuwa,uwekezaji huo si tu unadhihirisha uwezo mkubwa wa kampuni hiyo, bali pia unaonesha kuwa Tanzania ni sehemu salama na bora kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
“Tumefurahishwa sana na kile tulichokiona hapa Geita. GGML imewekeza kwa kiwango kikubwa sana katika teknolojia, usalama, na maendeleo ya kijamii. Hili ni jambo la kujivunia, na ni mfano mzuri tunaopaswa kuiga nchini Malawi,” amesema Khonje mara baada ya kutembelea mgodi huo.
Khonje ametumia fursa hiyo kuipongeza GGML kwa namna inavyoendesha shughuli zake kwa uwazi, ufanisi na kwa kuzingatia maslahi ya jamii inayozunguka mgodi huo.
Aidha, ameisifu Wizara ya Madini ya Tanzania kwa usimamizi thabiti unaoleta mafanikio ya kweli katika sekta hiyo nyeti.
“Tumekuja kujifunza na kuona namna Tanzania ilivyofanikiwa katika sekta ya madini. Ziara hii imetufungua macho kuona kuwa kuna mifumo bora ya usimamizi, uwazi na ushirikishwaji wa jamii, ambayo sisi Malawi tunaweza kuitekeleza kwa mazingira yetu,” ameongeza.
Katika ziara hiyo, ujumbe huo kutoka Malawi pia umetembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita na kukaribishwa rasmi na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Mohamed Gombati ambapo amesema kuwa, Tanzania na Malawi zimekuwa na uhusiano wa kihistoria wa muda mrefu, na kwamba ushirikiano kati ya nchi hizo unaendelea kuimarika katika nyanja mbalimbali ikiwemo uchumi, elimu na rasilimali madini.
“Tanzania na Malawi ni mataifa jirani yanayoshirikiana kwa karibu sana. Tunafarijika kuona kuwa mmeamua kutembelea Geita ili kujifunza. Tunaamini haya ni matunda ya ushirikiano wetu wa muda mrefu, na tunaendelea kuwakaribisha wakati wowote,” amesema Gombati.
Ujumbe huo pia umepata fursa ya kujifunza kuhusu mchango wa GGML katika maendeleo ya jamii, ikiwemo miradi ya afya, elimu, maji safi na uwezeshaji wa wajasiriamali kupitia mfumo wa uwajibikaji kwa jamii (CSR).
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Malawi katika kuimarisha sekta yake ya madini kwa kujifunza kutoka kwa nchi jirani zilizoendelea zaidi katika sekta hiyo, kwa lengo la kuboresha sera, mifumo ya usimamizi na kuvutia wawekezaji wa kimataifa.
Malawi inaweza kufaidika kwa kiasi kikubwa kwa kujifunza kutoka kwa Tanzania juu ya usimamizi bora wa sekta ya madini, ambayo imekuwa chanzo kikuu cha mapato na maendeleo ya kiuchumi.
Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa rasilimali za madini zinawanufaisha wananchi wake kupitia sera madhubuti, usimamizi wa uwazi, na uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa sekta ya madini, hatua hizi zinaweza kuwa mwongozo mzuri kwa Malawi, ambayo pia ina utajiri mkubwa wa madini, lakini haijafaidika ipasavyo na rasilimali hizo.
Miongoni mwa mafanikio makubwa ya Tanzania ni pamoja na kuanzishwa kwa sheria mpya za madini ambazo zimeongeza ushiriki wa serikali katika miradi ya madini.
Sheria hizo pia zimeweka mazingira ya kuwajibika kwa wawekezaji, huku wananchi wakihimizwa kushiriki moja kwa moja katika sekta hiyo, hasa kupitia uchimbaji mdogo mdogo uliorasimishwa.
Mbali na hayo, Tanzania imefanikiwa kuanzisha vituo vya biashara ya madini (mineral trading centers) ambavyo vimesaidia kuongeza uwazi katika ununuzi na uuzaji wa madini, pamoja na kuzuia utoroshwaji wa rasilimali hizo nje ya nchi.
Aidha,Malawi inaweza kujifunza kutokana na mfumo huo ili kuongeza mapato ya serikali na kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata masoko ya uhakika.
Pia, Tanzania imewekeza katika uongezaji thamani wa madini, ikiwa ni pamoja na usafishaji, ukataji na ung’arishaji wa vito.
Kwa msingi huo,Malawi inaweza kufuata nyayo hizo ili kuondokana na utegemezi wa kuuza madini ghafi pekee.
Taasisi kama Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) nchini Tanzania zimekuwa chachu ya ushiriki wa serikali katika miradi ya kimkakati, jambo ambalo limeongeza udhibiti wa rasilimali na mapato ya taifa.
Kwa ujumla, hatua za Tanzania zinaonesha kuwa sera thabiti, ushirikiano wa sekta binafsi na ya umma, pamoja na uwezeshaji wa wananchi katika sekta ya madini, ni msingi wa mafanikio ya kweli katika kutumia rasilimali za madini kwa maendeleo ya taifa.
Malawi, kwa nia ya dhati ya kisera na kisiasa, inaweza kufikia mafanikio kama hayo kwa kujifunza kutoka kwa Tanzania chini ya uongozi thabiti wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Tags
Habari
Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita
Makala
Sekta ya Madini Tanzania
Serikali ya Awamu ya Sita



