DAR-Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeendelea na jitihada za kuvutia wawekezaji kwa kuwaonesha fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya Miliki nchini.
Akizungumza katika kikao cha uwekezaji kilichofanyika Septemba 25, 2025 katika Ukumbi wa TBA jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri wa TBA, Arch. Wenceslaus P. Kizaba, amehimiza wawekezaji wa Kampuni ya Koeb Environmental Consult kutoka Nigeria kuja kuwekeza nchini.
Arch. Kizaba amesema Tanzania ni nchi yenye fursa nyingi za uwekezaji kwenye miradi ya ujenzi wa nyumba na majengo ya kisasa, hivyo TBA ipo tayari kushirikiana na wawekezaji wa kimataifa ili kuendeleza sekta hiyo.
Baadhi ya maeneo yanayotajwa kuwa na fursa za uwekezaji ni Canadian Masaki na Temeke Kota jijini Dar es Salaam, Ghana Kota jijini Mwanza, pamoja na miradi mingine ya nyumba katika mikoa ya Arusha na Geita.
