Makumbusho ya BoT yafungua milango kwa wananchi kufika kujifunza

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema, kupitia makumbusho yake wananchi wana nafasi ya kufika kupitia utaratibu uliowekwa na kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo historia ya benki hiyo na masuala mengine yanayohusu uchumi na fedha.
Hayo yamesemwa leo Septemba 16,2025 na Meneja Uhusiano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi.Vicky Msina wakati akizungumza na waandishi mbalimbali wa habari waliotembelea Makumbusho ya BoT iliyopo makao makuu ndogo jijini Dar es Salaam.

"Hii makumbusho imebeba historia iliyosheheni ya Benki Kuu ya Tanzania tulikotoka,tulipo na tunapoelekea.Watanzania hii ni makumbusho yenu, njooni mtajifunza historia ya Benki Kuu na nchi kwa ujumla.

"Utakapotembelea makumbusho yetu utajifunza mambo mbalimbali na tumeianzisha hii makumbusho ikiwa ni njia moja wapo ya kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala mbalimbali ya Benki Kuu, kuna wanafunzi mbalimbali wanakuja hapa kutaka kujua hali ya uchumi wetu tangu tulipopata Uhuru mpaka sasa ambapo kuna takwimu mbalimbali wanaonyeshwa."
Pia,Bi.Msina amesema, katika makumbusho hiyo wageni wanajifunza masuala ya noti na sarafu, machapisho mbalimbali, viongozi wa Benki Kuu tangu ilipoanzishwa mwaka 1966 mpaka sasa, matawi ya benki kuu na mengineyo.

Amesema, makumbusho hiyo inakuwa wazi siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri.

"Benki Kuu inawakaribisha wananchi wanaopenda kutembelea makumbusho hii kuwasilisha maombi yao kupitia barua pepe ya
botcommunications@bot.go.tz ambapo barua pepe hiyo itapokelewa na kujibiwa, na kupangiwa siku ili kutembelea makumbusho kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu Benki Kuu na masuala ya uchumi na fedha kwa ujumla."

Aidha, amesema tangu makumbusho hiyo ifunguliwe rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wananchi hususani wanafunzi wanaosoma masomo ya biashara kufika na kujifunza mambo mbalimbali.
Awali,Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa wa Benki Kuu, Bi.Lucy Shaidi amesema, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kupeperusha vyema bendera ya nchi kimataifa baada ya kutunukiwa Tuzo Kuu ya Ubunifu katika Huduma Jumuishi za Fedha (Nestor Espenilla Jr. Financial Inclusion Innovation Award).

Ni kutokana na utekelezaji madhubuti wa mifumo ya malipo ya kisasa, hatua inayochangia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za kufanya miamala kwa wananchi na kuongeza ufanisi wa huduma za kifedha nchini.

Tuzo hiyo ilipokelewa na Naibu Gavana anayesimamia Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Msemo, kwa niaba ya Gavana wa Benki Kuu, Bw. Emmanuel Tutuba, wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Huduma Jumuishi za Fedha uliofanyika mjini Swakopmund, nchini Namibia mwanzo mwa mwezi Septemba 2025.
Bi.Shaidi amewaeleza waandishi wa habari kuwa, tuzo hiyo mashuhuri imetolewa kwa kutambua mchango mkubwa wa Benki Kuu katika matumizi ya teknolojia na ubunifu katika kuongeza upatikanaji na utumiaji wa huduma rasmi za kifedha.

“Tuzo hii inaelenga kutambua nchi wananchama wa AFI ambao wameonesha jitihada kubwa katika ubunifu na matumizi ya teknolojia katika kutoa huduma jumuishi za kifedha kwa ajili ya kuchochea kasi ya upatikanaji na utumiaji wa huduma rasmi za fedha.”
Ameeleza kuwa, Benki Kuu imeibuka kidedea kufuatia utekelezaji madhubuti wa mfumo wa malipo ya papo kwa hapo yaani TIPS na namna ambavyo umesaidia kupunguza gharama kwa wananchi kufanya miamala kwa njia ya kidigitali.

Ameongeza kuwa, Benki Kuu imeonyesha mafanikio katika matumizi ya msimbo milia wa malipo (QR Code) unaofahamika kama TANQR unaowezesha wafanyabiashara nchini kupokea malipo ya bidhaa na huduma kwa njia rahisi kutoka kwa benki na kampuni za simu.

Amefafanua kuwa, mafanikio hayo yameiwezesha Tanzania kutambulika kimataifa, huku machapisho mbalimbali yakinukuu ubunifu wa BoT katika mifumo ya TIPS na TANQR, na kwamba nchi jirani ikiwemo Kenya, Rwanda, Uganda na Lesotho zimekuwa zikijifunza kutoka Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news