ZANZIBAR-Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia CCM, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ijayo itaongeza bajeti na kuwekeza zaidi katika kilimo na ufugaji ili wananchi wanufaike kiuchumi.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Septemba 16,2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Michezo Uzini huko Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.Amesema,wakulima watapatiwa pembejeo, mbegu bora, mbolea na masoko ya bidhaa zao kwa wakati.
Pia,wafugaji watawezeshwa mikopo isiyo na riba na kuunganishwa na masoko ya uhakika.
Vilevile,Dkt.Mwinyi amesema,mikopo midogo itawasaidia wananchi kuendeleza shughuli zao za uzalishaji.
Katika hatua nyingine, Dkt.Mwinyi amewataka wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujitokeza kwa wingi kupiga kura ifikapo Oktoba 29,2025 ili kuendelea kuleta maendeleo kwa Zanzibar.











