NA DIRAMAKINI
KATIKA hali ya kushangaza, mashabiki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DR Congo) wameharibu uwanja kwa kuvunja na kurusha viti eneo la kuchezea baada ya kichapo cha mabao 2-3 kutoka Senegal, ikiwa ni matokeo ya kushangaza zaidi.
Tukio hilo limetokea Septemba 9,2025 katika uwanja wa Stade des Martyrs ambao una uwezo wa kuhudumia mashabiki 80,000 kwa wakati mmoja Mjini Kinshasa.
Katika michuano hiyo ya kufuzu Kombe la Dunia kundi B,timu ya taifa ya DR Congo ilichapwa na Senegal nyumbani kwao, ikiwa ni ushindi wa kushangaza kwa Wasenegal.
Awali,DR Congo walikuwa wakiongoza 2-0 kabla bao hizo mbili kusawazishwa kisha wakaongezewa moja juu.
Cédric Bakambu dakika ya 26 aliiandikia DR Congo bao la kwanza, huku Yoane Wissa dakika ya 33 akiongeza la pili.
Matokeo yalikuwa ishara njema kwa DR Congo ingawa Idrissa Gana Gueye dakika ya 39 alianza kuharibu mipango baada ya kuipatia Senegal bao la kwanza.
Hadi kipindi cha kwanza kinatamatika, ubao ulikuwa unasoma mabao 2-1 ambapo katika kipindi cha pili dakika ya 53,Nicolas Jackson aliongeza bao la pili kwa Senegal na dakika ya 87,Mamadou Sarr alipashika bao la tatu ambalo liliwapa maumivu makali mashabiki wa DR Congo.
Senegal ina alama 18 huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikiwa na alama 16 katika kundi B.
