Mkakati wa Muda wa Kati wa Ukusanyaji wa Mapato wazinduliwa

DODOMA-Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba amezindua Mkakati wa Muda wa Kati wa Ukusanyaji wa Mapato wa Miaka Mitatu (Medium Term Revenue Strategy) uliopangwa kutekelezwa kuanzia mwaka 2025/2026 hadi 2027/2028 na Kamati za usimamizi na utekelezaji wa mkakati huo.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mkakati huo, ukumbi wa Kambarage Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma, Dkt. Mwamba alisema kuwa Mkakati huo unalengo la kuweka msingi imara ya ukusanyaji wa mapato, kuweka utabirifu wa sera za mapato na kuongeza makusanyo ya mapato.

Alisema kuwa utekelezaji wa Mkakati huo utasaidia kuongeza uhiari wa ulipaji kodi, kutambua na kuziba mianya ya ukwepaji kodi, kupunguza nakisi ya bajeti na kuimarisha imani ya wananchi na uwekezaji katika mfumo wa mapato.

“Utekelezaji wa kazi hii utaboresha usimamizi wa mapato ya Serikali na kuhakikisha tunakuwa na bajeti endelevu itakayowezesha Serikali kuongeza kasi ya utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi kwa kutumia mapato ya ndani,”alisema Dkt.Mwamba.
Dkt. Mwamba alisema kuwa, Mkakati umeainisha maboresho ya mikakati na hatua mbalimbali ambazo zimekuwa zikiendelea kutekelezwa na Serikali katika kuhakikisha Serikali inakusanya mapato mengi kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani.

Alisema kuwa hatua hizo zimegawanyika katika makundi matatu ambayo ni mapendekezo ya maboresho ya sera, maboresho ya usimamizi wa ukusanyaji wa mapato na maboresho ya Sheria.

Dkt. Mwamba alisema kuwa Mkakati huo ulioandaliwa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo washirika wa maendeleo na wadau wengine kutoka taasisi za Serikali na sekta binafsi, unapendekeza kuandaliwa kwa sera ya kodi kitaifa itakayotoa mwongozo wa kuandaa na kuboresha sera za kodi na kuboresha mifumo ya kielektroniki inayotumika katika ukusanyaji wa mapato.
Alisema kuwa, Mkakati huo utaongeza utii na uhiari wa ulipaji kodi, kuimarisha na kuboresha usajili wa walipakodi, kuboresha usimamizi wa misamaha ya kodi, kuboresha marejesho ya kodi, kuboresha viwango vya kodi, kuboresha na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato yanayotokana na uchumi wa kidigitali na kuboresha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato yanayotokana na forodha.

Kwa upande mwingine amewapongeza wajumbe wote walioteuliwa kwa kukubali uteuzi huo ili kushiriki katika kazi hiyo muhimu ambayo imejumuisha wajumbe wenye ujuzi na uzoefu katika masuala ya uchumi, kodi na fedha kutoka Serikalini na sekta binafsi.

Kwa upande wake Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Sera, Wizara ya Fedha, Dkt. Johnson Nyella, alisema kuwa uandaaji wa Mkakati ulianza na mashauriano yakiongozwa na wataalamu wa ndani na kisha Wataalamu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambao walitoa msaada wa kiufundi.

Alisema kuwa Mkakati huo ni muhimu katika kupunguza nakisi ya bajeti na hivyo kuwezesha kugharamia miradi ya maendeleo kwa kupitia fedha za ndani, lengo ni kuisaidia nchi kujitegemea ikizingatiwa Nchi imetoka uchumi wa chini kwenda uchumi wa kati ambao unahitaji kujitegemea kwa kiasi kikubwa.
Mwenyekiti wa Kamati iliyozinduliwa ni Katibu Mkuu Hazina na Katibu ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha anayesimamia Uchumi, Wajumbe wa Kamati ni pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Mipango na Uwekezaji, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii na Katibu Mkuu Wizara ya Mawasilino na Teknolojia ya Habari.

Wengine ni Gavana wa Benki Kuu, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Msajili wa Hazina, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, rais wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).
Utaratibu wa kuandaa na kutekeleza Mkakati huo umekuwa ukitumika katika nchi mbalimbali ikiwemo Kenya, Uganda, Malawi, Siera Leone, Ghana, Morocco na Rwanda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news