TBS yathibitisha mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, miaka minne ya ubora na ufanisi

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt.Ashura Katunzi amesema, ndani ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan,shirika hilo limepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake.
Ameyasema hayo leo Septemba 18,2025 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya wahariri na waandishi mbalimbali wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Aidha,ameishukuru ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuona umuhimu wa kuandaa kikao kazi hicho ili kuweza kuwasilisha mafanikio yao katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.

"Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lilianzishwa kama sehemu ya jitihada za Serikali katika kuimarisha miundombinu ya sekta za Viwanda na Biashara ili kukuza uchumi wa Taifa na linatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria ya Viwango Sura 130;
Afisa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw. Alex Malanga akiongoza kikao kazi hicho leo.

"Mafanikio hayo yameendelea kutimiza azma ya shirika katika masuala mbalimbali ili kutimiza matamanio ya wadau na Taifa kwa ujumla."

Dkt.Katunzi amesema, Serikali kupitia TBS inaendelea na juhudi za kuweka na kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuboresha huduma kwa lengo la kuwezesha biashara kwa madhumuni ya kuinua uchumi wa viwanda.

Ni kwa kuchagiza uzalishaji wa bidhaa salama na bora hapa nchini kama njia mojawapo ya kuchangia pato la Taifa.

"Hivyo,nichukue fursa hii kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi imara wa Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake na kuendelea kutusimamia na kuwa TBS hii mnayoiona hapa leo iking'ara kitaifa na kimataifa."

Dkt.Katunzi amesema, katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa ukaribu na kupunguza gharama, Serikali kupitia shirika hilo imeanza ujenzi wa maabara katika mikoa ya kimkakati ya Dodoma na Mwanza.
Amesema,ujenzi wa maabara hizo utagharimu jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 36.8 kati ya fedha hizo shilingi bilioni 24.7 ni kwa ajili ya Dodoma na shilingi bilioni 12.01 ni kwa ajili ya Mwanza.
Kwa upande wa Dodoma, amesema maabara zitakazojengwa zitahudumia mikoa mitatu ya Kanda ya Kati ambayo ni Dodoma, Singida na Tabora pamoja na mikoa mingine ya karibu.

Aidha, maabara za Mwanza zinatarajiwa kuhudumia mikoa sita, ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu.

Dkt.Katunzi amesema,pia shirika hilo limeshapata Mshauri Mwelekezi wa kuchora michoro ya jengo pamoja na kusimamia ujenzi wa maabara na ofisi jijini Arusha.

"Hatua hiyo ya ujenzi wa maabara itasaidia kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa majibu ya vipimo vya sampuli."
Vilevile, Dkt.Katunzi amesema, shirika hilo lina Kamati za Kitaalam (Technical Commitees) za Uandaaji Viwango 115 katika sekta ya chakula, kemikali, uhandisi mitambo, uhandisi umeme,

Uhandisi ujenzi, nguo na ngozi, madini na mitambo ya uchimbaji madini, mazingira na mtambuka (general tecniques).

Katika mchakato wa kuandaa viwango, amesema kamati hizo zinashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo vyuo vikuu, taasisi za utafiti, wafanyabiashara, wazalishaji, vyama vya walaji, vyama na bodi za wataalam, taasisi za udhibiti na watunga sera.
Dkt.Katunzi amesema,katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita,shirika limefanikiwa kuandaa viwango 2,765 vya sekta mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji ya soko ambavyo vitasaidia wafanyabiashara, wajasiriamali na watoa huduma kuzalisha bidhaa bora zenye kukidhi matakwa ya viwango.

Lengo ni kuwawezesha kufanya biashara ndani na nje ya nchi, hatua ambayo italeta tija na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Aidha,amesema jumla ya vyeti na leseni za ubora 3,184 vimetolewa kwa wazalishaji, miongoni mwao wakiwemo wajasiriamali wadogo 1,359.
"Serikali kupitia TBS imekuwa ikitenga zaidi ya TZS milioni 350 kila mwaka kwa madhumuni ya kuhudumia wajasiriamali wadogo bila ya malipo yoyote.

"Leseni hizi zimesaidia wazalishaji kuweza kuzalisha bidhaa bora, ikiwa ni pamoja na bidhaa zao kuweza kuaminika sokoni na pia kufanya biashara nje ya mipaka ya Tanzania, hivyo kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa."

Mbali na hayo, Dkt.Katunzi amesema,shirika hilo limeendelea na huduma za usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi pamoja na maeneo ya uzalishaji, uuzaji, usambazaji na uhifadhi wa chakula.
Sambamba na vipodozi kwa lengo la kuhakiki ubora na usalama wa maeneo hayo ili kuendelea kulinda afya za walaji ambapo jumla ya bidhaa 8,199 zilisajiliwa na maeneo 47,886 yalisajiliwa.

Pia, katika kuimarisha ukaguzi wa bidhaa mbalimbali zinazoingia nchini kutoka nchi za nje, amesema TBS huhakiki ubora wa bidhaa na magari yaliyotumika kabla ya kusafirishwa kuja nchini ambapo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita jumla ya shehena za bidhaa 153,159 zilikaguliwa.

Ni kabla ya kuingia nchini kupitia mfumo wa Pre-Shipment to Conformity (PVoC) na shehena za bidhaa 352,103 zilikaguliwa baada ya kufika nchini kupitia mfumo wa Destination Inspection (DI).

"Aidha, jumla ya magari 203,689 yalikaguliwa. Bidhaa hizi zinakaguliwa kwa lengo la kuiepusha Tanzania kuwa jalala la bidhaa duni pamoja na kulinda afya, usalama na mazingira ya watumiaji."
Kwa upande wa mafunzo,Dkt.Katunzi amesema,TBS imetoa mafunzo kwa jumla ya wadau 5,437 wakiwemo wazalishaji wa bidhaa za viwandani na wasindikaji.

Mafunzo hayo amesema yalihusu dhana nzima ya viwango na ubora ambayo yatawawezesha kuzalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango na yamewawezesha kupata uelewa mpana kwenye masuala ya udhibiti ubora, hivyo kuwaandaa kuhimili ushindani wa masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.

Vilevile, amesema kupitia Mradi wa Qualitan TBS na SIDO mwaka 2024 waliwezeshwa kutoa mafunzo kwa wazalishaji wa bidhaa za chakula 1000 katika mikoa 10 ikiwemo Dar es Salaam, Singida, Mwanza, Geita, Kagera, Kigoma, Shinyanga, Tanga, Ruvuma na Kilimanjaro.
"Na TBS imeendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali ili kukuza uelewa juu ya masuala ya viwango na udhibiti ubora.

"Njia hizo ni pamoja na kushiriki katika makongamano, maonesho,warsha na semina, kuandaa mikutano na wadau wa masuala ya viwango, kutoa mafunzo mbalimbali kuhusu masuala ya ubora na usalama na kuendesha kampeni za elimu kwa umma katika ngazi za wilaya."

Aidha, amesema elimu imekuwa ikitolewa kupitia vyombo vya habari zikiwemo redio jamii, redio za kitaifa,runinga, magazeti, mitandao ya kijamii,matangazo, majarida na vipeperushi.
Wakati huo huo, Dkt.Katunzi amesema,TBS ina jumla ya maabara 12 na zote zimeweza kupata ithibati za umahiri, ambapo maabara hizo zimehakikiwa na kupatiwa vyeti vya ithibati ya umahiri wa kimataifa.

"Hatua hiyo inamaanisha kuwa majibu ya sampuli kutoka katika maabara hizo yanaaminika kokote duniani na hivyo kurahisisha biashara ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu.

"Katika kipindi hicho TBS imeweza kupima sampuli zaidi ya 152,812 na kufanyia ugezi vifaa 42,993 ambapo suala hili litasaidia kuhakikisha katika soko kunakuwa na bidhaa zenye ubora.

"Maabara za TBS zina mashine za kisasa (state-of -art-equipment) zinazopelekea kupata majibu kwa wakati na sahihi, Serikali imeweza kutumia kiasi kisichopungua shilingi bilioni 12.9 kuhakikisha mashine hizi zinapatikana."

Pamoja na mashine nyingi zilizopo katika maabara hizo, Dkt.Katunzi amesema, kuna mashine za kipekee ikiwemo ya hydrostatic pressure test ya kupima mabomba ya maji na yenye uwezo wa kupima mabomba yenye kipenyo cha milimita 12 sawa na inchi 0.5 hadi milimita 800 sawa na inchi 32.
Amesema,mashine hiyo ina uwezo pia wa kupima sampuli 120 kwa wakati mmoja na kati ya nchi 54 za barani Afrika inapatikana katika nchi tano tu ikiwemo Tanzania.

"Mashine ya automatic conductor resistance tester ya kupimia waya (cables) za umeme za aina zote zenye kipenyo hadi kufikia milimita 40 sawa na milimita za mraba 1200.

"Mashine hii ni ya kipekee kwa kuwa ni ya kidigitali na ina uwezo wa kupima na kutoa majibu kwa haraka."

Kuhusu mashine ya solar simulator, Dkt. Katunzi amesema, katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati inapatikana Tanzania pekee katika ofisi za TBS.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema,mashine hiyo ina uwezo wa kupima solar panels za aina zote bila kutegemea uwepo wa jua.

Wakati huo huo, Dkt.Katunzi amefafanua kuwa, shirika hilo limeendelea kuonesha umahiri mkubwa, hivyo kupata tuzo za Kimataifa.

"Mnamo mwaka 2023, TBS ilipata mafanikio makubwa kwa kushinda tuzo ya kuwa Mdhibiti Bora Barani Afrika kwa Mwaka 2023."

Amesema,tuzo hiyo inaonesha dhamira ya TBS katika utendaji bora na mchango wake chanya katika kukuza viwango na kudhibiti ubora.

Vilevile, amesema TBS imekuwa taasisi ya kwanza katika Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kupata ithibati ya mifumo ya udhibiti ubora wa bidhaa ya kimataifa katika wigo mpana ndani ya muda mfupi.

"Na ni ya taasisi ya tatu kupata ithibati hiyo iliyotolewa na SADCAS mwezi Septemba, 2024 hivyo kufanya mifumo hiyo kutambulika kimataifa.
"Pia kwa mwaka 2025, TBS imefanikiwa kupata ithibati ya umahiri wa mfumo wa usimamizi wa chakula katika kiwango cha kimataifa toleo jipya (ISO 22003:2022).

"Kuhamia kwenye ithibati hii kunaifanya TBS kuwa taasisi ya kwanza katika Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kupiga hatua hiyo.

"Ithibati hii ni ishara kuwa TBS inafanya kazi zake kwa kuzingatia miongozo ya kimataifa iliyowekwa na hivyo kuendelea kuaminiwa na wateja na wadau wengine

"TBS pia tunajivinua kuwa na wataalam wenye umahiri na weledi mpaka kutambulika kimataifa, kwani wataalam wa TBS hualikwa na SADCAS kwa ajili ya kutoa msaada wa kitaalam."

Dkt.Katunzi amesema, ni katika masuala ya ithibati kwenye maeneo ya Metrolojia, uthibitishaji wa ubora na ukaguzi kwa taasisi na mashirika yanayohitaji huduma hizo katika Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Aidha, amesema shirika hilo kupitia wataalam wake liliweza kutoa Mshindi wa ISO Next Generation Award kwa mwaka 2023.
Dkt.Katunzi amesema,tuzo hiyo iliandaliwa na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO) ambayo ilikuwa na lengo la kutambua mchango wa wataalam katika kuandaa viwango vinavyochagiza maendeleo endelevu ya kimataifa (UN SDGs).

"Shindano hili lilihusisha maafisa viwango wenye umri chini ya miaka 35 kutoka nchi takribani 175 wanachama wa ISO na mtaalam kutoka TBS aliibuka mshindi na kukabidhiwa tuzo husika huko Brisbane nchini Australia," amebainisha Dkt.Katunzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news