Msajili wa Hazina aipa tano TPA

TANGA-Msajili wa Hazina, Bw.Nehemiah Mchechu ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) hususani Bandari ya Tanga kwa ufanisi mzuri wa kukusanya mapato makubwa ikiwa ni matokeo ya kukamilika kwa mradi wa maboresho katika bandari hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa Septemba 1,2025 na Msajili wa Hazina wakati wa ziara yake katika bandari hiyo kwa lengo la kukagua utendaji kazi wake.

Akiongea mara baada ya kupokea taarifa ya utendaji kazi wa bandari hiyo, Bw. Mchechu amesema kuwa,uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan uliogharimu kiasi cha shilingi bilioni 429.1 umewezesha meli kubwa kuweza kutia nanga na shehena ya mzigo pamoja na mapato kuwa makubwa.

"Tutahakikisha kuwa sekta binafsi pamoja na sekta ya umma zinaungana katika kufanya uwekezaji mkubwa kwa ajili ya manufaa ya umma."
Aidha, Bw. Mchechu amewataka wafanyakazi wa Bandari ya Tanga na TPA kwa ujumla kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuwataka kuiona bandari hiyo kama eneo muhimu la Serikali katika uchumi wa nchi.

“Lakini pia niwasihi wafanyakazi wa bandari hii tuone ufahari, kwani tupo sehemu ambayo ni jicho na mboni ya Serikali katika uchumi wa nchi, hivyo lazima tuichukulie kama sehemu muhimu inayohitaji huduma zilizo bora na tija kwa ajili ya maendeleo,“amesema Mchechu.

Pia, Msajili wa Hazina amesema, kufanya kazi kwa bidii kutawezesha mapato kuongezeka na mapato yakiongezeka hata gawio la taasisi za umma litaongezeka,kwani malengo ni kufikia shilingi trilioni 2.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, Bw. Plasduce Mbossa amesema kuwa, uwekezaji uliofanyika katika Bandari ya Tanga umesaidia kuhudumia meli gatini kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake Meneja wa Bandari ya Tanga Bw. Masoud Athumani Mrisha alimhakikishia Msajili wa Hazina kuwa huduma katika Bandari ya Tanga itazidi kuimarika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news