ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amehimiza kuimarishwa kwa diplomasia ya uchumi kati ya Zanzibar na Japan, ili kukuza ushirikiano wa kimaendeleo na kuongeza fursa za uwekezaji visiwani.
Dkt. Mwinyi ametoa wito huo leo Septemba 9,2025 alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mheshimiwa Anderson Gukwi Mutatembwa, katika ukumbi wa Ikulu, Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa, Japan ni miongoni mwa mataifa yenye wawekezaji wengi wenye uzoefu na teknolojia ya kisasa, ambao Zanzibar inawakaribisha kuwekeza hususani katika maeneo ya uchumi wa buluu, biashara ya mwani, utalii, michezo, pamoja na utafiti wa mafuta na gesi.Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesema,Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalenga kuanzisha viwanda vya kuchakata na kuzalisha bidhaa zitokanazo na rasilimali za baharini, jambo linalohitaji ushirikiano wa karibu na nchi marafiki kama Japan katika kuvutia wawekezaji wa kimkakati.
Kwa upande wake, Balozi Mutatembwa amemhakikishia Rais Dkt.Mwinyi kuwa, Ubalozi wa Tanzania nchini Japan utaendelea kusimamia kwa dhati utekelezaji wa ajenda za maendeleo na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Japan, ikiwemo fursa maalum kwa Zanzibar katika miradi ya kimkakati.




