ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi amejumuika na waumini wa Dini ya Kiislamu, ndugu, jamaa na marafiki katika hafla ya khitma ya kumuombea kaka yake, marehemu Abbas Ali Mwinyi.
Hafla hiyo imefanyika Septemba 27,2025 katika Msikiti wa Jamia Zinjibar uliopo Mazizini, Mkoa wa Mjini Magharibi, ambapo waumini mbalimbali walihudhuria kwa lengo la kushiriki dua na kuonesha mshikamano wa kidugu katika kipindi hiki cha majonzi.
Hotuba na dua maalum ziliongozwa na masheikh pamoja na viongozi wa dini waliotoa nasaha kuhusu umuhimu wa kumuombea marehemu na kuendeleza mshikamano wa familia na jamii.
Aidha, hafla hiyo imeambatana na utoaji wa sadaka ya chakula kwa waumini wote waliohudhuria kama sehemu ya kuendeleza mila na desturi za Kiislamu katika matukio ya namna hii.
Rais Dkt.Mwinyi amewashukuru wote waliofika kushiriki khitma hiyo, akisisitiza thamani ya mshikamano na upendo katika wakati wa huzuni, akisema kuwa moyo wa faraja unaotolewa na jamii unaleta faraja kubwa kwa familia.
Marehemu rubani Abbas Ali Mwinyi ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu marehemu Ali Hassan Mwinyi, na kaka wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Mwinyi alifariki Septemba 25,2025 akipatiwa matibabu Hospitali ya Lumumba Mjini Unguja. Aidha, alizikwa Septemba 26,2025 huko nyumbani kwa Mangapwani.Licha ya marehemu Abbas Ali Mwinyi kukumbukwa kama mtu mpole, mwenye upendo na mshikamano na jamii yake kabla ya umauti wake alikua msemaji wa familia mara baada ya kifo cha Baba yao.
Abbas Ali Hassan Mwinyi alikuwa mwanasiasa Mtanzania na mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alichaguliwa kuwa Mbunge wa Fuoni kwa mwaka 2015-2025.Pia, Abbas alikuwa msomi, rubani wa ndege na nahodha wa meli. Marehemu alikuwa tena mgombea ubunge wa Jimbo la Fuoni kupitia CCM.
















