GEITA-Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, amepongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa jitihada zake za kuelimisha umma kuhusu masuala ya fedha na uchumi kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.
Mhandisi Zena alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la BoT, ambapo alipokelewa na Meneja wa Idara ya Mawasiliano BoT, Bi. Victoria Msina. Katika maelezo yake, Bi. Msina alieleza kwa kina huduma zinazotolewa na wataalamu wa BoT kwa wananchi wanaotembelea banda hilo.







