NA LWAGA MWAMBANDE
REJEA katila neno la Mungu kupitia Biblia Takatifu kitabu cha Zaburi 117:1–2 inasema, “Msifuni BWANA,enyi mataifa yote; mtukuzeni, enyi watu wote. Kwa maana upendo wake kwetu sisi ni mkuu,na uaminifu wa BWANA ni wa milele. Msifuni BWANA.”
Pia,kusifu ni kuonesha kuabudu au kukubali, tunamsifu Bwana kwa sifa zake, kazi zake, na tabia yake.Sifa ni pamoja na matendo ya kubariki, kupongeza,kuheshimu,kushukuru, kusherehekea,na kushangilia.
Aidha,tunamsifu Bwana kwa sababu anastahili sifa zetu zote.Anastahili kuabudiwa na kibali chote.
Pia rejea, Zaburi 103:1-2...Ee nafsi yangu, mhimidi Bwana, na vyote vilivyo ndani yangu na vilihimidi Jina lake takatifu. Ee nafsi yangu, mhimidi Bwana, Wala usisahau faida zake zote.”
Zaburi 150:6...Kila kilicho na pumzi na kimhimidi Bwana. Haleluya!”
Isaya 12:4...Na siku hiyo mtasema,mshukuruni Bwana, liitikeni jina lake; tangazeni matendo yake katikati ya mataifa, litajeni jina lake kuwa limetukuka.”
Wafilipi 2:9-11...“Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu, kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.”
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasema, kusifu jina la Bwana ni agizo la kiroho na furaha ya mtu aliye na imani.
Vilevile, ni tendo la moyo linalomwelekeza Mungu katika kila hali ya maisha,wakati wa furaha na hata katika mateso.
Kwa hiyo, tumsifu Bwana daima, kwa kuwa yeye ni mwaminifu na jina lake ni la ajabu.Endelea;
1. Ee nafsi yangu sikia, mimi ninakusemesha,
Ukisikiza tulia, nipate kuelewesha,
Si kukimbiakimbia, heri ukanikosesha,
Nasifu jina la Bwana, ambalo ni takatifu.
2. Vitu vyote ndani yangu, viwe vya kumwadhimisha,
Huo ni wajibu wangu, jinsi ananiwandisha,
Fadhili za kwake kwangu, sitajisahaulisha,
Nasifu jina la Bwana, ambalo ni takatifu.
3. Ninakosa asamehe, huyu wa kumwadhimisha,
Kwangu nifanye sherehe, za Mungu kumvumisha,
Iwe kwa zote tarehe, bila muda kukatisha,
Nasifu jina la Bwana, ambalo ni takatifu.
4. Magonjwa naumwaumwa, mwili yanadhoofisha,
Ni kama mwili nalimwa, kwa mwili kunitingisha,
Maombi kwake yatumwa, afya anaihuisha,
Nasifu jina la Bwana, ambalo ni takatifu.
5. Kaburi likitishia, kutaka kunitowesha,
Kati anaingilia, kuyakomboa maisha,
Nakwenda nafurahia, sababu aningárisha,
Nasifu jina la Bwana, ambalo ni takatifu.
6. Taji ya fadhili Bwana, kwa rehema anivisha,
Nguvu kutoka ujana, uzee anifikisha,
Ninayo amani sana, jinsi ananiwandisha,
Nasifu jina la Bwana, ambalo ni takatifu.
7. Bwana ni mfanya haki, kuonewa anafisha,
Azidi kunibariki, pazuri anifikisha,
Nafsi zidi mlaiki, jinale ukivumisha,
Nasifu jina la Bwana, ambalo ni takatifu.
8. Hatutendi sawasawa, vile tunavyomwangusha,
Hatulipi sawasawa, jinsi tunavyochemsha,
Nafsi acha kuchachawa, mema ukanikosesha,
Nasifu jina la Bwana, ambalo ni takatifu.
9. Rehema za Mungu kwetu, nini tutafananisha,
Ukuu wa Mungu kwetu, nini tutalinganisha,
Atukuzwe Mungu wetu, milele pasipokwisha,
Nasifu jina la Bwana, ambalo ni takatifu.
10. Jina lako Mungu wetu, sana umelipaisha,
Hufananishwi na kitu, ulivyojikamilisha,
Wewe kila kitu kwetu, ndivyo twakuadhimisha,
Nasifu jina la Bwana, ambalo ni takatifu.
11. Nikuheshimu Muweza, katika yote maisha,
Nizidi kukutuza, imani nikidumisha,
Kwa sababu unaweza, yote unakamilisha,
Nasifu jina la Bwana, ambalo ni takatifu.
(Zaburi 103:1-11)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602