GEITA-Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigela ametembelea banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwenye Maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya EPZ Bombambili, mkoani Geita. Maonesho hayo yanafanyika kuanzia Septemba 18 hadi 28, 2025.
Katika ziara yake, Mhe. Shigela alipatiwa maelezo kuhusu ushiriki wa Benki Kuu kwenye maonesho hayo, ambao unalenga zaidi kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake ya msingi katika kusimamia uchumi wa taifa. Miongoni mwa majukumu hayo ni kuhifadhi akiba ya fedha za kigeni na dhahabu.
Hadi kufikia Agosti 2025, Benki Kuu ilikuwa imenunua jumla ya tani 9.165 za dhahabu zenye thamani ya takribani Dola za Marekani milioni 1,015.98, hatua inayochangia kuimarisha hifadhi ya taifa na kudumisha uthabiti wa uchumi.


