NA LWAGA MWAMBANDE
UKIREJEA katika neno la Mungu kupitia Biblia Takatifu kuanzia Agano la Kale hadi Agano Jipya, utaona neno la Mungu linahimiza kwamba mtu aliyepewa jukumu la kumwakilisha Mungu, kumtumikia na kuangalia watu wake, anapaswa kuwa mwaminifu, makini na mwenye moyo wa kuwahudumia wengine kwa upendo na uadilifu.

Pia,kama wakili wa Mungu,unahitajika kutenda haki na kusema ukweli kila wakati,hata kama watu hawatakupenda. Hii ni kama msaidizi mwaminifu ambaye hufanya kazi yake kwa moyo wote,bila kujibadilisha au kukwepa majukumu.
Kwa kuwa unajua kwamba Mungu anakutazama, unapaswa kuwa mwaangalifu zaidi katika maneno na matendo yako. Jukumu lako si la kawaida, bali ni kubwa na muhimu.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, kama unajua mengi kuhusu Mungu na kweli yake, basi unapaswa kuwahudumia wengine kwa hekima na upendo zaidi,kwani maarifa yako yanakuweka kwenye kiwango cha juu cha uwajibikaji.Endelea;
1. Uwe ni kielelezo, katika maisha yako,
Uufanye mwendelezo, yasemavyo maandiko,
Ujue hicho kigezo, kwa watu na Mungu wako,
Wewe wakili wa Mungu, umuwakilishe vema.
2. Yesu ni kielelezo, tushikao maandiko,
Yeye awe ni kigezo, kote kule tuendako,
Tusiufanye mchezo, tofauti zikaweko,
Wewe wakili wa Mungu, umuwakilishe vema.
3. Jinsi tunavyomwamini, kushika yake kuweko,
Hapo twaupa thamani, wito wake ulioko,
Naye atatuamini, maongezeko yaweko,
Wewe wakili wa Mungu, umuwakilishe vema.
4. Mtu awaye yeyote, kudharau kusiweko,
Katika maisha yote, nenda na heshima yako,
Akutafutetafute, asipate doa kwako,
Wewe wakili wa Mungu, umuwakilishe vema.
5. Kwa waaminio wote, kuiga kwako kuweko,
Wasioamini wote, wakuone wa mashiko,
Ulipo pale popote, ububujike upako,
Wewe wakili wa Mungu, umuwakilishe vema.
6. Katika usemi wako, toa ya kimaandiko,
Na hata mwenendo wako, upendo kwako uweko,
Imani usafi wako, wasiwasi usiweko,
Wewe wakili wa Mungu, umuwakilishe vema.
7. Maneno yenye uzima, toka kwake Mungu wako,
Hayo uzidi yasema, matendo mema yaweko,
Wote wale walokwama, kufunguliwa kuweko,
Wewe wakili wa Mungu, umuwakilishe vema.
8. Yesu ni kielelezo, mwinginewe asiweko,
Yale yake makatazo, utii kwako uweko,
Aliokupa uwezo, kuyatumia kuweko,
Wewe wakili wa Mungu, umuwakilishe vema.
9. Atutendeavyo Bwana, kuigaiga kuweko,
Na sisi tuzidi sana, kuyaishi maandiko,
Tulipo paweze nona, upako uwe ujiko,
Wewe wakili wa Mungu,umuwakilishe vema.
10. Sasa kazi ya wakili, uaminifu uweko,
Yeye aishike kweli, na kujituma kuweko,
Yoyote yale dhalili, kwake huyo yasiweko,
Wewe wakili wa Mungu, umuwakilishe vema.
11. Tambua wewe barua, inasomwa kote huko,
Mungu ukimuinua, hiyo heri njema kwako,
Naye atakutambua, sasa hadi mwisho wako,
Wewe wakili wa Mungu, umuwakilishe vema.
(1 Timotheo 4:12, 2, Tito 2:7, 2 Wakorintho 3:2)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602