DAR-Young Africans Sports Club (Yanga SC) imeendelea kuonesha ubabe katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika (CAFCL),baada ya kutinga raundi ya pili ya ligi hiyo.

Ni baada ya kupata ushindi wa jumla wa mabao 5-0 dhidi ya Williete SC ya Angola ikishinda 3-0 ugenini katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa Ijumaa ya Septemba 19, 2025 katika dimba la The Estádio 11 de Novembro (Estádio Nacional 11 de Novembro) nchini Angola.
Mabao hayo yalifungwa na Aziz Andambwile dakika 31,Edmund John dakika 71 na Prince Dube akakamilisha bao la tatu dakika 79 ya mchezo huo.
Aidha,Septemba 27,2025 Yanga SC katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam iliishindilia Williete SC mabao 2-0.
Mabao ya Yanga SC dhidi ya Williete SC yalifungwa na Pacome Zouzoua dakika ya 70 huku bao la pili likifungwa dakika ya 86 na Aziz Andabwile.
Kwa matokeo hayo, Yanga SC itachuana na Silver Strikers ya Mali iliyotinga raundi ya pili kwa goli la ugenini kufuatia sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Elgeco PIus kabla ya sare ya 0-0 kwenye marudiano.






