Tanzania yashuhudia kupatwa kwa Mwezi leo Septemba 7,2025

NA DIRAMAKINI

LEO Septemba 7, 2025 Tanzania imeshuhudia kupatwa kwa Mwezi Kikamilifu (Umbra) ikiwa ni miongoni mwa matukio adimu zaidi angani.
Tukio hili la angani limeonekana mwezi ukiwa na rangi nyekundu kwa muda mrefu.

Septemba 6,2025 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilifafanua kuwa,hali ya kupatwa kwa Mwezi ni tukio linalotokea wakati Dunia inapita kati ya Jua na Mwezi na kusababisha kivuli cha Dunia kuwa katika uso wa Mwezi.
Aidha, hali hii hutokea wakati Dunia, Mwezi na Jua vinapokaa kwenye mstari mnyoofu. "Tukio la kupatwa kwa mwezi limegawanyika katika aina kuu mbili.

"Aina ya kwanza ni kupatwa kwa Mwezi Kikamilifu (Umbra), hali ambayo Dunia inakuwa imefunika mwanga wote wa Jua na kupelekea kivuli kizito (giza) katika uso wa Mwezi.

"Aina ya pili ni kupatwa kwa Mwezi Sehemu (Penumbra) ambapo Dunia husababisha kivuli hafifu katika uso wa Mwezi."
TMA ilibainisha kuwa,tukio la kupatwa kwa Mwezi kwa Septemba 7, 2025 ni la kupatwa kwa Mwezi Sehemu na Kikamilifu.Tukio hili limeshuhudiwa katika maeneo ya bara la Ulaya, Asia, Australia na Afrika.

Kwa hapa nchini, hali ya kupatwa kwa Mwezi ilianza kwa kupatwa kwa Mwezi Sehemu kuanzia Jua lilipozama hadi saa 2:29 usiku na kufuatiwa na kupatwa kwa Mwezi Kikamilifu kuanzia saa 2:30 hadi saa 3:52 usiku.
TMA ilibainisha kuwa, kwa kawaida, mzunguko wa mwezi una uhusiano mkumbwa na Kupwa na Kujaa kwa maji baharini.

Hali hii imetarajiwa kuongezeka kwa kina cha maji katika Bahari wakati wa tukio hilo. Hata hivyo, hali hiyo haikurajiwa kupekelea athari kubwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news