TCB yaamua kugawa utajiri kwa wananchi kupitia Stawi Bond, yarekodi mafanikio makubwa kupitia mageuzi ya ndani

NA GODFREY NNKO

BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imezindua rasmi hatifungani mpya ya miaka mitano ijulikanayo kama Stawi Bond ambayo inatoa riba ya kuvutia ya asilimia 13.5 kwa mwaka na itakuwa inalipwa kila baada ya robo ya mwaka.
Uzinduzi huo umefanyika leo Septemba 17,2025 jijini Dar es Salaam huku wajasiriamali wadogo na wa kati ambao mara nyingi hukumbana na changamoto za upatikanaji wa mitaji wakitarajiwa kunufaika kwa mikopo ya riba nafuu kote nchini.

Hatua hiyo imefikiwa, baada ya Mamlaka ya Mitaji na Masoko ya Dhamana (CMSA) kuidhinisha waraka wa matarajio wa programu ya miaka mitano ya hatifungani hiyo yenye jumla ya shilingi bilioni 150.
Pia, katika toleo la kwanza CMSA imeidhinisha TCB Stawi Bond yenye jumla ya shilingi bilioni 50 huku kiwango cha chini cha kuwekeza ikiwa ni shilingi 500,000.

Akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi katika hafla hiyo ambaye alitarajiwa kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt.Doto Biteko, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya amesema kuwa,uzinduzi wa TCB Stawi Bond ni hatua muhimu nchini inayoashiria safari ya Tanzania ya kuendelea kukuza na kuimarika kwa masoko ya mitaji nchini.

Naibu Katibu Mkuu huyo amesema,hatua hiyo inatoa fursa pana kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika uwekezaji wa kitaifa nchini.
"Tuchukue fursa hii, kuwapongeza TCB kwa hatua hii ya kishujaa, kuwa mstari wa mbele kutafuta ufumbuzi makini wa changamoto tulizonazo.”

Amesema, kupitia hatifungani ya Stawi, TCB itaongeza uwezo wake wa kutoa mikopo ya muda mfupi na muda mrefu kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Naibu Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa, hatua hiyo itawawezesha wajasiriamali kupata mikopo yenye riba nafuu ambayo itawasadia kushiriki kikamilifu katika uzalishaji.

“Uzinduzi wa Stawi Bond ya Benki ya TCB ni hatua muhimu inayounga mkono dhamira ya Serikali kupitia Wizara ya Fedha ya kupanua masoko ya mitaji nchini.”

“Hatifungani hii, siyo tu ni chombo cha kifedha cha kuwekeza bali pia ni njia ya kuimarisha ushiriki wa wananchi katika uwekezaji wa Kitaifa yaani Financial Inclusion.”
Amesema, pia itasaidia kupunguza utegemezi wa mikopo ya kigeni na kuongeza mapato ya Serikali. Kupitia hatua hiyo, Naibu Katibu Mkuu huyo amesema,Wizara ya Fedha inaona mchango mkubwa katika utekelezaji wa sera za kifedha hususani kuongeza ushirikishwaji wa kifedha na kukua uchumi shirikishi nchini.

Pia,amesema, Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za kifedha kuhakikisha kwamba, bidhaa kama hizo za Stawi Bond zinaendelea kuanzishwa na kufanikisha Dira ya Taifa ya ukuaji uchumi endelevu.

“Wizara ya Fedha ina dhamana ya kusimamia sera za fedha na uchumi nchini,moja ya malengo makuu ya sera hizo ni kupunguza utegemezi wa mikopo ya gharama kubwa kutoka nje na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika kugharamia maendeleo ya nchi yao kupitia uwekezaji wa ndani.
Afisa Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Bw.Adam Mihayo amesema, hilo ni tukio muhimu na la kihistoria kwa Benki ya TCB ambayo inaadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1925.

"Tukaona tusherehekee miaka hii 100 kwa kuja na ubunifu na kuja na bidhaa ambayo kwanza itapanua wigo wa ku-mobilze ukwasi pamoja na mtaji ambao utatuwezesha ku-drive ajenda ya financial Inclusion na kuleta fursa ya kukuza uchumi wetu."

Amesema, hatifungani ya TCB Stawi Bond ni maalumu kwa ajili ya ku-mobilze ukwasi na mtaji kwa ajili ya kuunga mkono wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Amesema,biashara ndogo na za kati zimekuwa na mchango mkubwa nchini,kwani zinachangia zaidi ya asilimia 30 ya uchumi nchini.

"Lakini,pia uapozungumzia biashara 10, tisa kati ya hizo ni biashara ndogo na za kati, kwa hiyo tukiweza kuwasapoti hawa tutakuwa tunafungua fursa za ajira na kupanua wigo wa Serikali kukusanya mapato na mapato haya yanaenda moja kwa moja kwenye shughuli za maendeleo."

Pia, amesema kutokana na mabadiliko makubwa ambayo yanaendelea kufanyika ndani ya Benki ya TCB, wameanza kushuhudia matokeo makubwa.

Amesema, kwa mwaka 2020/2024 mali za benki ziliongezeka madhubuti kwa asilimia 25 kutoka trilioni 1.4 hadi trilioni 1.7.
“Mwaka huu, mpaka mwezi wa saba benki yetu imefanikiwa kukuza jumla ya mali kwa asilimia tisa, kutoka trilioni 1.7 hadi trilioni 2.1 mwezi wa nane.”

Amesema, ukuaji huo ni mkubwa kuliko wastani wa ukuaji wa benki 14 kubwa hapa nchini, ambazo zina mali ya zaidi ya trilioni moja.

Mtendaji Mkuu huyo amesema, ukuaji huo unawapa faraja kuona maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi yanaonesha njia.

Vilevile, amesema, amana za wateja ikiwa ni kiashiria kizuri cha uaminifu, kwa mwaka 2020/2024 benki hiyo ilifanikiwa kuongeza amana za wateja kutoka trilioni 1.1 hadi trilioni 1.3 ikiwa ni sawa na ukuaji wa asilimia 16.

Aidha, amesema, mwaka 2020/25 hadi mwezi Agosti amana zao zimekuwa kutoka trilioni 1.3 hadi trilioni 1.6 sawa na ukuaji wa asilimia 23 ikiwa ni ukuaji wa juu zaidi ya benki 14 nchini ambazo zilikuwa kwa asilimia 16 pekee.
“Ninawashukuru sana wateja kwa imani kubwa mnayotupa TCB," amesema huku kwa upande wa mikopo, Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema, mwaka 2020/2024 mikopo imekuwa kutoka trilioni 0.9 hadi trilioni 1.1 sawa na ukuaji wa asilimia 25.

Amesema, takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zilionesha ukuaji wa mikopo kwa mwaka 2020/24 kwa sekta binafsi ilikuwa ni asilimia 13.

Amesema, ukilinganisha na wao. Asilimia 25 inaonesha wazi kuwa,wanaendelea kukuwa,kwani hadi kufikia mwezi Agosti, mwaka huu mikopo yao imefikia trilioni 1.3 sawa na ukuaji wa asilimia 19.

Amesema, takwimu za Benki Kuu zinaonesha kuwa, ukuaji wa mikopo kwa kipindi hicho ilikuwa ni asilimia 16.

“Kingine ambacho kinatupa faraja ni kwamba, wakati tunaanza safari hii ya mageuzi, asilimia 80 ya mikopo yetu ilikuwa inatolewa kwa watumishi wa Serikali na wastaafu.
“Lakini, sasa tunayo furaha kusema kwamba, mpaka mwisho wa mwezi Agosti,mwaka huu mikopo ambayo tumetoa kwa wafanyabiashara ambayo inaenda moja kwa moja kwenye sekta za uzalishaji ni asilimia 44 ambazo zimekuwa kwa zaidi ya asilimia 55 mwaka hadi mwaka.
Amesema, wataendelea kuunga mkono zaidi sekta za uzalishaji ili ziendelee kuleta matokeo bora kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Kuhusu mikopo chechefu amesema, kwa TCB imeendelea kuwa chini ya kiwango kilichowekwa na Benki Kuu kwani, hadi Agosti mwaka huu mikopo yao chechefu ni asilimia 3.8 ambayo ni chini ya kiwango cha BoT.

Upande wa faida, amesema, mwaka 2020/2024 benki hiyo ilitengeneza faida ya shilingi bilioni 44 kabla ya kodi ikilinganishwa na mwaka mmoja kabla hawajaanza mageuzi hayo ambapo walipata hasara.
“Na kwa kweli mwaka huu, baada ya miaka mingi tumetoa gawio kwa Serikali na kwa wenye hisa la bilioni tano, kwa hiyo endeleeni kutupa sapoti, miaka ijayo tutafanya vizuri zaidi.”

Kwa mwaka huu hadi mwezi Agosti, amesema TCB imetengeneza faida ya shilingi bilioni 33 kabla ya kodi huku wakitarajia mwaka huu kupata faida ya zaidi ya shilingi bilioni 50.

Kuhusu kiwango cha faida kwa mtaji wa hisa kwa mwaka jana amesema,ilikuwa ni asilimia 21. Afisa Mtendaji Mkuu huyo ameishukuru Serikali chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwani, mwaka 2023 baada ya kufanya consolidation, Serikali iliwapa mtaji wa shilingi bilioni 131.

“Na lazima, nikiri kuwa, mtaji ule umejenga msingi imara wa utendaji huu ambao mnauona.Pili niwashukuru sana wateja wetu,kwa thamani kubwa ambayo mmekuwa mkituonyesha ndani ya hii miezi 18 toka tuanze kutekeleza huu mkakati mpya na wafanyakazi wetu wote kwa utendaji kazi uliotukuka.”

CMSA

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama amesema, Stawi Bond ni ya kihistoria kwa kuwa ni mara ya kwanza benki ya Serikali kutoa hatifungani ya aina hiyo.
Pia, amesema thamani ya masoko ya mitaji nchini imeendelea kukua kwa kasi,kwani katika kipindi cha miaka minne imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 75 kutoka trilioni 31.64 mwaka 2021 hadi kufikia trilioni 55.45 mwezi uliopita.

DSE

Naye Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Peter Nalitolela amesema,Stawi Bond imezinduliwa kwa wakati muafaka,kwani sasa wananchi wanaweza kuwekeza kwa urahisi kupitia mifumo ya kidigitali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news