TPBA yaendelea kuwa jukwaa muhimu kwa mawakili wa Serikali

NA GODFREY NNKO
Dodoma

CHAMA cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) kimeendelea kuwa jukwaa muhimu kwa mawakili wa Serikali katika kuhakikisha kinaendelea kusimamia maadili ya kitaaluma kwa wanachama wao ili kuimarisha hadhi ya taaluma ya sheria nchini.
"Ndiyo maana huwezi kusikia mawakili wa Serikali wametoka nje na kusema hiki na kile hovyo, kwa sababu tuna maadili yetu ndani ya chama kwa mujibu wa misingi na kanuni za utumishi wa umma."

Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania, Bavoo Junus ameyasema hayo leo Septemba 12,2025 katika siku ya pili ya kikao kazi kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wahariri mbalimbali wa vyombo vya habari nchini ndani ya Ukumbi wa Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dodoma.

TPBA kimeanzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 16A(1) cha Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura 268 na Tangazo la Serikali Na. 589 la tarehe 16 Agosti 2019.

Pia, amesema chama kimeendelea kuwa nguzo muhimu katika kusimamia, kutetea, kupigania na kulinda maslahi ya Taifa na rasilimali zake tofauti na mawakili binafsi ambao huwa wanalinda maslahi ya wateja wao.

"Lakini, pia tuna jukumu la kuelimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo sheria, kutoa huduma za msaada wa kisheria na hili limefanyika kwa mafanikio makubwa hasa kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia,"amesema Rais Junus ambapo kampeni hiyo inafanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema, TPBA ambacho ni chama cha kitaaluma kinawaunganisha wanasheria wote waliopo katika ofisi za umma au utumishi wa umma kwenye halmashauri, wizara, wakala, taasisi mbalimbali, kampuni ambazo Serikali ina hisa na kwingineko.
"Kama wakili hayupo ofisi ya umma, huyo hawezi kukidhi vigezo vya kuwa mwanachama wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania.

"Kwani, mawakili wa Serikali popote walipo wanamsaidia Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku,kwa sababu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndiye mshauri mkuu wa masuala yote ya sheria yanayohusu Serikali."

Amesema, lengo kubwa la chama hicho ni kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali yanayohusu masuala ya kitaaluma na kuangazia namna ya kuishauri Serikali kuhusu mambo ya sheria na katiba.

"Lakini, mawakili wa Serikali huwa hawachagui kufanya kazi, popote wapo, ukienda halmashauri, wapo, manispaa wapo, mikoa wako, wametawanyika nchi nzima tofauti na wenzetu ambao wanapanga wenyewe wafanye kazi maeneo gani, lakini mawakili wa Serikali wapo nchini nzima."
Amesema, kupitia umoja huo wametengeneza jukwaa kwa ajili ya kuwaungainsha mawakili wa Serikali wajadili mambo yao yanayohusiana na taaluma za kisheria, kutetea maslahi ya Serikali, kwani mi mawakili wa umma ambao mteja wao mkuu ni Serikali.

"Pia, kuna malengo mengine mahususi ikiwemo kupokea maoni ya wanachama ambao kila mmoja ana maoni yake ambayo yakikusanywa vizuri yatasaidia Serikali katika kutekeleza mipango yake.

Vilevile, kusaidia katika kukuza ufanisi wa mfumo wa sheria nchini, uelewa na kutoa mafunzo endelevu kwa wanachama wao badaa ya kusubiri waajiri wafanye hivyo.

Rais huyo amesema, katika kipindi cha miaka miwili ya chama hicho wamepata mafanikio makubwa ikiwemo kutoa misaada ya ushauri wa kisheria kwa wananchi bure.

"Na tumeendelea kutoa elimu ya sheria kupitia vyombo mbalimbali vya habari, kuandaa makongamano ya kisheria yenye lengo la kukuza uelewa wa jamii na wananchi kwa ujumla kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu sheria."
Mafanikio mengine, amesema ni kuandaa mafunzo mahususi kwa lengo la kujenga na kuimarisha uwezo wa wanachama na kushiriki karika huduma mbalimbali za kijamii.

Kuhusu tofauti iliyopo kati ya Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Rais Junus amesema kuwa, TPBA ni chama cha kitaaluma cha wanasheria wanaohudumia Serikali pekee.

"TLS ni chama cha kitaaluma cha wanasheria wote nchini bia kujali mwajiri kwa maana ya Serikali au sekta binafsi. Uanachama ndani ya TPBA unategemea uendelevu wa ajira ya mwanachama husika katika utumishi wa umma, kwa upande wa uanachama ndani ya TLS hauna muda maalumu wa ukomo,"amefafanua Rais huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news