NA DIRAMAKINI
MHESHIMIWA Dkt.Hussein Ali Mwinyi alipoingia madarakani mwishoni mwa mwaka 2020, uongozi wake kupitia Serikali ya Awamu ya Nane iliweka mkazo mkubwa katika Uchumi wa Buluu.
Uchumi ambao haukuwekewa mkazo mkubwa miaka ya nyuma kama alivyofanya kupitia uongozi wake, ni uchumi ambao unajumuisha utalii, uvuvi, bandari, mwani, mafuta na gesi.
Wengi wetu, tulimchukulia poa kwa msimamo wake kupitia uchumi wa buluu bila kutambua kuwa, maono yake kupitia uchumi huo yameangazia mbali zaidi kwa mustakabali wa uchumi wa wananchi Zanzibar na Taifa kwa ujumla.
Sasa, tuliokuwa tunamchukulia poa, tunakiri wazi kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi, Zanzibar imepiga hatua kubwa katika kuimarisha dhana ya uchumi wa buluu.
Ikiwa ni mfumo wa maendeleo unaotegemea utajiri wa rasilimali za baharini na pwani kwa ajili ya kukuza uchumi wa taifa, kuboresha maisha ya wananchi na kulinda mazingira ya bahari.
Rais Dkt.Mwinyi ameonesha dhamira ya dhati kwa kuipa sekta hii kipaumbele cha kipekee.
Moja ya mafanikio makubwa ni kuongezeka kwa uzalishaji wa samaki, ambapo tani zilizovuliwa zimeongezeka mara dufu katika kipindi cha miaka mitano.
Aidha,thamani ya sekta ya uvuvi nayo imeongezeka maradufu, ikichochewa na uboreshaji wa miundombinu kama bandari ndogo, madiko, masoko ya kisasa ya samaki na uwekezaji katika teknolojia za kisasa za uvuvi.
Katika sekta ya mwani, Zanzibar imejipatia heshima kimataifa kama mzalishaji mkubwa wa zao hilo, linaloajiri zaidi ya asilimia 90 ya wanawake katika maeneo ya pwani.
Kupitia sera ya uchumi wa buluu, serikali imefanikiwa kuongeza uzalishaji maradufu huku kukijengwa kiwanda cha kisasa cha kusindika mwani huko Pemba chenye uwezo wa kusindika tani 30,000 kwa mwaka.
Zaidi ya hayo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua hatua madhubuti katika kuongeza maarifa na utaalamu wa kitaalamu kupitia ujenzi wa vituo vya mafunzo ya baharini, ushirikiano na taasisi za utafiti kama Taasisi ya Sayansi za Baharini (IMS), pamoja na kuanzisha utaratibu wa utoaji wa vitalu vya baharini kwa wawekezaji binafsi.
Hatua hizi zimefungua milango ya uwekezaji katika sekta ndogo kama ufugaji wa samaki, kilimo cha mwani, usindikaji wa bidhaa za baharini na hata utafutaji wa mafuta na gesi asilia baharini.
Kwa misingi hiyo, ni vyema kuipongeza Serikali ya Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa ujasiri na ubunifu wake katika kulipa uzito suala la uchumi wa buluu.
Ikumbukwe,hili ni somo la uongozi unaoona mbali unaopambana na changamoto kwa vitendo,na kuweka msingi wa maendeleo endelevu kwa ustawi bora wa jamii na Zanzibar mpya.
Hivyo, Zanzibar ina kila sababu ya kujivunia uongozi unaoacha alama chini ya Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi.
Ndiyo maana,Oktoba mwaka huu kila mmoja wetu ana wajibu wa kuendeleza jitihada hizi kwa ari mpya,ufanisi zaidi na mshikamano wa kitaifa kwa kumpa kura za ushindi wa kishindo Dkt.Hussein Ali Mwinyi ili akamalizie kutekeleza yaliyomo katika Uchumi wa Buluu.
Dkt.Mwinyi anaamini kuwa,uchumi wa buluu si tu ndoto, bali ni njia halisi ya kupunguza umaskini,kukuza ajira na kulinda mazingira. Ni jukumu letu sote kuhakikisha mafanikio haya yanadumu na mwenye kuyadumisha zaidi ni mwasisi wake Dkt.Hussein Ali Mwinyi.
Oktoba hii hatutaki porojo, tunataka vitendo. Na kwa vitendo tulivyoona, kura yetu ni kwa Dkt.Mwinyi na CCM. Ametuonesha mwelekeo wa uchumi wa kisasa, sasa tunakwenda kumuongezea mwendo akatekeleze zaidi.