NA DIRAMAKINI
MHESHIMIWA Dkt.Hussein Ali Mwinyi tangu aingie madarakani Novemba, 2020 kama Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameleta mabadiliko mabadiliko makubwa ya kisiasa, kijamii na kiuchumi visiwani,hususani kisiwani Pemba.
Wananchi wa Pemba, ambao kwa miaka mingi walihisi kuwa pembezoni kimaendeleo na kisiasa, sasa wanaonesha wazi upendo, imani na matumaini makubwa kwa uongozi wa Dkt. Mwinyi.
Ikumbukwe kuwa, moja ya mafanikio makubwa ya awali ya Dkt.Mwinyi ni hatua yake ya kisiasa ya kuleta maridhiano.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi alichukua hatua ya kujenga serikali ya umoja wa kitaifa kwa kushirikisha vyama vya upinzani ikiwemo ACT-Wazalendo.
Maridhiano hayo yameleta utulivu wa muda mrefu Pemba, ambako kwa miaka mingi kulikuwepo na misuguano ya kisiasa iliyoathiri maendeleo.
Kwa, sasa wananchi wa Pemba wamehisi kuthaminiwa siyo tu kama sehemu ya Zanzibar, bali kama mshirika kamili wa maendeleo na ustawi wa Taifa.
Jambo hili limeongeza upendo na imani yao kwa Rais Dkt.Mwinyi wakimuona kama kiongozi wa haki, mwenye kuleta maelewano, na mshikamano katika jamii.
Pia,katika kipindi kifupi cha uongozi wake,Dkt. Mwinyi amesimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kisiwani Pemba ikiwemo nishati, ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya barabara inayorahisisha shughuli za usafirishaji, maboresho ya sekta ya afya,elimu, kilimo na mingineyo.
Miradi hii haikuishia kwenye makaratasi, bali utekelezaji wake unaonekana kwa macho na kushuhudiwa na wananchi.
Hakika, hakuna njia bora ya kujenga imani ya wananchi kama kuwaonesha maendeleo yanayoathiri maisha yao moja kwa moja.
Vilevile, Dkt.Mwinyi aliweka wazi msimamo wake dhidi ya vitendo vya rushwa, uzembe, na ubadhirifu wa mali ya umma.
Kupitia kaulimbiu yake ya Zanzibar ya Viwanda na Uchumi wa Buluu, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameweka mkazo kwa viongozi wa umma kuwajibika na kuhakikisha huduma bora kwa wananchi.
Hali hii imejenga heshima na upendo miongoni mwa wananchi wa Pemba ambao kwa muda mrefu walikuwa wakihitaji uongozi unaojali wananchi zaidi ya siasa.
Kwa msingi huo, wananchi Pemba wanamuona Dkt.Mwinyi si kama kiongozi wa chama kimoja, bali kama rais wa watu wote.
Aidha,tofauti na viongozi wengi waliopita,Dkt. Mwinyi ameonesha kuwa karibu sana na wananchi wa kawaida.
Mara kwa mara ameshiriki mikutano ya hadhara, kusikiliza kero za wananchi moja kwa moja na kutoa maelekezo ya haraka kwa viongozi husika kuzitatua.
Hii imempa sura ya uongozi unaojali na kusikiliza, jambo ambalo linaongeza mapenzi na heshima kwake miongoni mwa wananchi kote Unguja na Pemba.
Chini ya uongozi wa Dkt.Mwinyi, hali ya kisiasa imekuwa shwari na ya matumaini kote Zanzibar.Wananchi wanajivunia kuwa sehemu ya taifa linaloelekea kwenye mwelekeo sahihi wa maendeleo bila migogoro ya mara kwa mara.
Ni wazi kuwa, upendo wa wananchi wa Pemba kwa Dkt.Mwinyi haukuja kwa bahati mbaya. Ni matokeo ya uongozi uliojaa hekima, usikivu, uwajibikaji, na dhamira ya kweli ya kujenga Zanzibar ya haki na usawa.
Dkt.Mwinyi ameandika ukurasa mpya katika historia ya siasa na maendeleo ya visiwa hivi viwili vya Unguja na Pemba.
Katika mioyo ya wengi, hasa wananchi wa Pemba, Dkt.Mwinyi si tu Rais, bali ni kiongozi wa matumaini, mshikamano na mabadiliko ya kweli, mpenda haki na msimamizi wa maendeleo ya watu.Tukutane Oktoba.
