ARUSHA-Viongozi wa vyama vya ushirika wa mazao bustani Wilaya ya Karatu Mkoa wa Arusha wametakiwa kuwajibika na kuwa wabunifu kwa kutoa huduma mbalimbali kwa wanachama ili kuimarisha ushirika ikiwemo kusaidia kupata soko la pamoja, pembejeo za kilimo na mikopo.
Aidha, wamesistizwa kuanzisha huduma mbalimbali zikiwemo uujazi wa mbolea zitakazowasaidia wanachama na hata kuwavutia wananchi wengine kujiunga na vyama vyao.
Hayo yameelezwa Agosti 30,2025 na Kaimu Naibu Mrajis-Uratibu na Uhamasishaji, Consolatha Kiluma alipofanya ziara wilayani humo ili kuona maendeleo ya vyama hivyo ikiwa ni pamoja na kusikia changamoto na maoni kwa ajili ya kuboresha na kuimalisha ushirika.
Amesema kuwa, viongozi wa vyama wanahitaji kuhamasisha wananchi kujiunga kwa kuwa sehemu ya utoaji huduma hasa mbolea, kwani huo ndio msingi wa kuwa na ushirika.
Aidha, wameelekezwa kuwa na mfuko wa fedha wa chama ili kujiendesha na kutoa huduma bora kwa wanachama wao kwa kuanzisha vyanzo mbalimbali.
"Mnahitaji kuwa wabunifu, kwa kuanzisha vyanzo vya mapato ili kukuza mtaji wa chama ili kutoa huduma bila changamoto kwa wanachama," amesema Kiluma.
Viongozi wa vyama hivyo wameipongeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kufanya ziara hiyo, kwani imewasaidia kufikisha changamoto ambazo haikuwa rahisi kutokana na mazingira yao.
Vyama vilivyotembelewa ni Mang'ola Amcos Ltd, Laghangareri Amcos Ltd na Jobaj Amcos Ltd ambavyo vyote wanachama wake wanajishughulisha na kilimo cha vitunguu.
