Wananchi waguswa na huduma za Bodi ya Bima ya Amana (DIB) maonesho ya Madini

GEITA-Wananchi mbalimbali wametoa maoni yao walipotembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana (DIB) katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mjini Geita, wakieleza kufurahishwa na elimu wanayoipata kuhusu usalama wa amana zao katika taasisi za kifedha nchini.
Maonesho hayo ambayo yamekusanya wadau kutoka sekta ya madini, fedha, teknolojia na huduma nyingine, yamekuwa jukwaa muhimu kwa taasisi kama Bodi ya Bima ya Amana (DIB) kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake ya kulinda amana za wateja katika mabenki yanayoshiriki kwenye mfumo wa bima ya amana nchini.

Akizungumza mara baada ya kutembelea banda hilo, mmoja wa wakazi wa Geita, amesema, "Sikujua kama kuna chombo kinacholinda fedha zetu iwapo benki itapata changamoto. Kupitia maelezo niliyopata hapa, nimeelewa kuwa kuna usalama zaidi katika kuweka fedha benki."

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa DIB, Bw.Lwaga Mwambande amesema, lengo kuu la ushiriki wao kwenye maonesho hayo ni kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu uwepo wa bima ya amana na namna inavyofanya kazi.

"Tunataka wananchi waelewe kuwa fedha wanazoweka kwenye taasisi za kifedha zilizosajiliwa zinalindwa hadi kiwango fulani iwapo taasisi hizo zitashindwa kuendelea na huduma."

Maonesho hayo yalianza Septemba 18,2025 na yanatarajiwa kuendelea hadi Septemba 28,2025 yakitoa fursa kwa wananchi na wadau mbalimbali kujifunza na kushiriki mijadala ya kitaalamu kuhusu maendeleo ya sekta ya madini na huduma zinazoiunga mkono.

Kuhusu DIB

Miongoni mwa majukumu ya Bodi ya Bima ya Amana ni kutathmini na kukusanya michango kutoka benki na taasisi za fedha zinazopokea amana, na kusimamia Mfuko wa Bima ya Amana, kukinga amana za wateja na kulipa fidia wenye amana endapo benki au taasisi ya fedha itaanguka au kufilisika.
DIB pia ina wajibu wa kufanya ufilisi wa benki au taasisi ya fedha iliyoshindwa kuendelea na biashara ya huduma za kibenki au iliyofilisika endapo ikiteuliwa na Benki Kuu ya Tanzania kama mfilisi.

Aidha, kuanzia Julai mwaka huu, DIB imeongezewa jukumu la kushiriki katika kupunguza hasara kwa benki au taasisi ya fedha inayotetereka.

Bodi ya Bima ya Amana ilianzishwa kwa Mujibu wa Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya Fedha ya mwaka 1991 na kuanza kufanya kazi mwaka 1994.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here