RAILA Amolo Odinga ameondoka akiwaacha wafuasi wake na Wakenya kwa ujumla wakiwa na majonzi mengi.
Ni kati ya viongozi mahiri waliokuwa na msimamo thabiti wa kuziendea ndoto zake za kuwaongoza Wakenya katika ngazi ya Urais, licha ya mikwamo na vigingi vingi,aliendelea kuonesha nia.
Rejea katika kumbukumbu utaona, Raila alijitosa kwenye kinyang’anyiro cha urais katika miaka ya 1997, 2007, 2013, 2017 na 2022, lakini ndoto yake ya kuingia Ikulu haikutimia na alitarajia 2027 kuwania tena.
Kwa takribani miongo minne, Raila alikuwa na ufuasi mkubwa kote nchini, na jina lake lilikuwa na ushawishi wa kipekee katika siasa za kila uchaguzi mkuu nchini humo.
Kampeni nyingi nchini ziliundwa ama kwa kumuunga mkono au kwa kumpinga, ingawa za kumuunga mkono Baba zilikuwa na nguvu zaidi nchini Kenya.
Wafuasi wake walivutiwa na misimamo yake ya mageuzi, na msimamo wake wa kuwatetea wanyonge, hasa kutoka jamii zilizohisi kunyanyaswa na tawala zilizopita ambazo mara nyingi zilihusisha makabila mawili makuu nchini.
Katika uchaguzi mkuu wa 2007, Raila aliingia ulingoni kama mgombea aliyeonekana kuungwa mkono sana, na alipoteza kwa tofauti ndogo dhidi ya Rais wa wakati huo, Mwai Kibaki, katika uchaguzi uliobishaniwa sana.
Matokeo ya uchaguzi huo yalisababisha ghasia mbaya zaidi za baada ya uchaguzi kuwahi kushuhudiwa nchini Kenya, ambapo zaidi ya watu 1,000 waliuawa na maelfu wakakimbia makazi yao.
Wafuasi wake waliamini kuwa aliibiwa ushindi. Chama chake cha ODM kilipata viti vingi bungeni, kikimshinda Kibaki ambaye alikuwa akiwania kwa tiketi ya Party of National Unity (PNU).
Kupitia mazungumzo ya amani yaliyoongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, marehemu Kofi Annan, Raila aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu katika serikali ya mseto iliyoanzishwa ili kurejesha utulivu.
Aidha, kutokana na matokeo hayo yaliyoonekana kumuumiza zaidi Raila Amolo Odinga tarehe 30 Januari,2018 akiwa kiongozi wa Muungano wa Upinzani wa NASA, alijiapisha kuwa rais wa jamhuri ya watu wa Kenya mbele ya wafuasi wake katika bustani ya Uhuru jijini Nairobi.
Katika uchaguzi wa 2022, Raila tena alionekana kuwa miongoni mwa wagombea waliopigiwa upatu kushinda, safari hii akiungwa mkono na Rais aliyekuwa madarakani, Uhuru Kenyatta, ambaye alikuwa ameachana na Naibu Rais wake, William Ruto.
Kwa wafuasi wake, huo ulikuwa wakati mwafaka wa Raila kuingia Ikulu, hasa kutokana na uungwaji mkono wa serikali na ufuasi wake wa jadi. Lakini kwa mara nyingine tena, alishindwa na Dkt.William Ruto, ambaye alipata asilimia 50.49 ya kura dhidi ya asilimia 48.85 za Raila.
Raila alipinga matokeo hayo katika Mahakama ya Juu zaidi nchini Kenya, lakini jopo la majaji saba liliidhinisha ushindi wa Dkt.William Ruto.
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, Raila Amolo Odinga ameondoka bila kutimiza ndoto yake ya Urais, lakini...Endelea;
1. Amekufa na kinyongo, ndivyo wengi twaamini,
Kutotinga kwa ulingo, alivyokwenda vitani,
Mambo yalifanywa fyongo, kumkandamiza chini,
Kweli hapa duniani, hivipati vyote vyako.
2. Nasema kwenye siasa, alivyokuwa makini,
Kama mtu wa hamasa, ikulu pawe nyumbani,
Lakini amepakosa, hadi kwenda kaburini,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
3. Raila jela lifungwa, hata kwenda ugenini,
Jinsi alisongwasongwa, kwamba abakie chini,
Licha ya kote kupingwa, lizidisha upinzani,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
4. Chaguzi za vyama vingi, na yeye mashindanoni,
Alivyoupiga mwingi, angelifika enzini,
Lakini vingi vigingi, akabaki pembezoni,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
5. Hadi akajiapisha, tena mbele hadharani,
Hasira akaonesha, kotekote duniani,
Wapi kulimfikisha, hakufika kileleni,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
6. Licha ya kuwa pembeni, wala si serikalini,
Hakubaki asilani, kubwaga manyanga chini,
Lizidi kuwa kazini, hadi kufika mwishoni,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
7. Raila na wengi wafu, wameenda kaburini,
Pamoja na kuwasifu, wanafaa kileleni,
Kama kura ya turufu, hawakutinga kitini,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
8. Yabaki historia, ya Raila duniani,
Alivyotutumikia, hata kukawa amani,
Pale alipoingia, tukaishi kivulini,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
9. Kwao aliitwa baba, heshima kubwa jamani,
Kwa wengine huyo baba, aliushika mpini,
Akisema walishiba, hata kwenda mzigoni,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
10. Unayoyatekeleza, ukiwapo duniani,
Ndiyo yatakueleza, ukitoka duniani,
Vema ukajiongoza, ubakie midomoni,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
11. Raila ameondoka, toka kwetu duniani,
Jinsi aliwajibika, anabaki maishani,
Mema yake tutashika, hasa kusaka amani,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
12. Angelikuwa Rais, muda Fulani zamani,
Ila hakuwa Rais, ni mambo ya duniani,
Taasisi ya Rais, kupata ngumu jamani,
Kweli hapa duniani, huvipati vyote vyako.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
