NA LWAGA MWAMBANDE
HIVI karibuni Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza mpango wa kusitisha mapigano kati ya Israel na kundi la Hamas, lengo ni kukomesha mauaji na mateso ya raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.
Picha na Reuters.Mpango huu unalenga kuanzisha hali ya utulivu kwa muda wa siku 60, kutoa misaada ya kibinadamu kwa raia wa Gaza na kuwezesha mazungumzo ya muda mrefu ya amani.
Hatua hii imekuja kufuatia ongezeko la shinikizo la kimataifa juu ya Marekani na Israel kutokana na idadi kubwa ya vifo vya raia na uharibifu mkubwa wa miundombinu.
Rais Trump alitangaza kuwa Israel imekubali awamu ya kwanza ya mpango wake, ambayo inajumuisha kusitisha mashambulizi, kubadilishana mateka na kuruhusu upatikanaji wa misaada ya kibinadamu chini ya usimamizi wa kimataifa.
Mpango huu pia unapendekeza uundwaji wa kikosi cha kimataifa kitakachosimamia utekelezaji wa makubaliano na kutoa mafunzo kwa vikosi vya usalama vya Palestina.
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasema kuwa, licha ya mapungufu ambayo Rais Trump wengi wanaona anayo katika uongozi wake, kwa mpango huu wa kusitisha mapigano huko Gaza ni jambo muhimu ambalo linapaswa kuungwa mkono na kuliombea kwa Mungu ili lifanikiwe kikamilifu.Endelea;
1. Trump ni mtu mbaya, kwake afukuza watu,
Asema pasipo haya, wageni waondoke tu,
Walakini siyo mbaya, hiki amefanya kitu,
Mauaji kule Gaza, kachangia kukomesha.
2. Miaka yote miwili, watu wanauana tu,
Wa karibu na wa mbali, libaki tunalia tu,
Ilikuwa mbaya hali, waangamiavyo watu,
Mauaji kule Gaza, kachangia kukomesha.
3. Yeye siyo malaika, kwamba atende vvema tu,
Mengine anachemka, sawa tukimsema tu,
Lakini hili hakika, amekonga roho zetu,
Mauaji kule Gaza, kachangia kukomesha.
4. Pengine hatujafika, kuridhisha wale watu,
Yapo ya kulalamika, kwamba kiini macho tu,
Kafanya tumeridhika, vyakoma vifo vya watu,
Mauaji kule Gaza, kachangia kukomesha.
5. Moja ya ahadi zake, alisema huyu mtu,
Ya kwamba kwa mbinu zake, vita vyote viishe tu,
Twampa kongole zake, hakuna vifo vya watu,
Mauaji kule Gaza, kachangia kukomesha.
6. Imani inasogea, atufaa huyu mtu,
Licha mengi kukosea, la Gaza ni jema kwetu,
Uhai ametetea, mengine yatakuja tu,
Mauaji kule Gaza, kachangia kukomesha.
7. Pengine na Ukraine, vita vyaweza kwisha tu,
Ya kwamba wasipigane, na wazidi kufa watu,
Hilo jema tulione, linazo faida kwetu,
Mauaji kule Gaza, kachangia kukomesha.
8. Rais Trump heko, jinsi unajali watu,
Kuliko mitikisiko, kwamba yote ikome tu,
Amani pate kuweko, inayotufaa watu,
Mauaji kule Gaza, kachangia kukomesha.
9. Trump uje na Afrika, nako wauana watu,
Kwingikwingi vyasikika, vita na vifo vya watu,
Ni wazi ukitamka, amani takuweko tu,
Mauaji kule Gaza, kachangia kukomesha.
10. Kweli ncha ya upanga, siyo ya amani kwetu,
Wakatanao mapanga, mwisho kukaa chini tu,
Hoja waweze kujenga, na amani iwe yetu,
Mauaji kule Gaza, kachangia kukomesha.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602