Awamu ya Sita ilivyoipandisha chati Tanzania mapambano dhidi ya rushwa Afrika

NA GODFREY NNKO 

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeonesha dhamira thabiti na mikakati madhubuti katika vita dhidi ya rushwa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Bw. Crispin Chalamila kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 27 Machi, 2025. (Picha na Ikulu|Maktaba).

Aidha, jitihada zake kuanzia mageuzi ya sera, kuimarisha taasisi hadi kuhimiza uwazi na uwajibikaji zimezaa matunda yanayotambulika kimataifa.

Tanzania sasa inajivunia mafanikio makubwa ambayo si tu yameimarisha mazingira ya biashara na utawala wa haki, bali pia yameipa nchi heshima na sifa katika viwango vya kimataifa vinavyopima mapambano dhidi ya rushwa.

Aidha,Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amekuwa akiwaonya wala rushwa wa kimataifa na kuwataka watambuwe kwamba nchi yake si mahala salama kwao kujificha na kuendeleza vitendo vya kifisadi na utakatishaji fedha. "Tanzania si chaka la wala rushwa..."

Rais Dkt.Samia aliyasema hayo katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mapambano dhidi Rushwa barani Afrika yaliyofanyika jijini Arusha Julai 11, 2023 na kuhudhuriwa na viongozi wa taasisi za rushwa kutoka nchi mbalimbali za Afrika.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, kiongozi huyo wa Tanzania alisema,nchi yake si kichaka cha kuficha fedha za rushwa na wala si salama kwa wala rushwa.

Ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na Shirika la Transparency International ya Corruption Perceptions Index (CPI) ya mwaka 2024, inaonesha kuwa,Tanzania imepanda katika orodha katika udhibiti wa rushwa.

Kupitia ripoti hiyo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshika nafasi ya pili katika nchi za Afrika Mashariki na ya 14 barani Afrika.

Ni wazi kuwa,mafanikio katika suala la udhibiti wa rushwa hapa nchini hayakuja bila juhudi za makusudi na mikakati madhubuti ambayo Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikitekeleza chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia.

Aidha,mafanikio haya ni matunda ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), sekta za umma, binafsi na wananchi kwa ujumla.

Katika ripoti hiyo ya Shirika la Transparency International, Tanzania imepata alama 40 kati ya 100, ikiwekwa katika nafasi ya 87 kati ya nchi 180 duniani zilizohusishwa katika ripoti.

Haya ni maendeleo makubwa ikilinganishwa na alama ya 38 iliyopatikana mwaka 2023, ambapo Tanzania ilikuwa katika nafasi ya 94 duniani, ambapo katika ripoti ya mwaka 2024, imeongeza alama mbili na kupanda kwa nafasi saba katika kipindi kifupi.

Katika ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania inashika nafasi ya pili baada ya Rwanda, ambayo ilipata alama 53 na kushika nafasi ya 49 duniani.

Hii inamaanisha kuwa, Tanzania imepiga hatua za kubwa katika kuboresha uwazi na utawala bora na kuwa kielelezo kwa nchi nyingine barani Afrika.

Mfano katika ripoti hiyo Uganda ina alama 26, hivyo kushika nafasi ya 14 huku Kenya ikipata alama 31 na kushika nafasi ya 126 duniani.

Ukirejea ripoti za nyuma utabaini kuwa, maendeleo ya Tanzania katika kupambana na rushwa ni makubwa na yanaendelea kutia moyo kwa ustawi bora wa jamii na Taifa.

Mathalani mwaka 2020, Tanzania ilikuwa na alama 38 katika ripoti iliyotolewa na Shirika la Transparency International ya Corruption Perceptions Index (CPI) na mwaka 2021 alama ziliongezeka hadi 39.

Aidha, miaka ya 2022 na 2023 alama zilishuka hadi 38, lakini mwaka 2024 imepanda hadi kufikia alama 40.

Prof.Mkumbo

Kwa matokeo hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema,Tanzania imeendelea kupiga hatua katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, jambo linalothibitishwa na takwimu hizo za kimataifa.

Akizungumza hivi karibuni katika Jukwaa la Cafetalk lililofanyika, Prof.Mkumbo amesema, kwa mujibu wa vipimo vya Transparency International, Tanzania inashika nafasi ya pili katika Afrika Mashariki kwa juhudi za kupambana na rushwa, ikitanguliwa na Rwanda.

“Kwa vipimo vya Transparency International vinavyopima mwenendo wa rushwa duniani, Tanzania ni ya pili kwa Afrika Mashariki kwenye kupambana na rushwa, tumebaki nyuma ya Rwanda pekee.

"Ndani ya Afrika, sisi ni wa 14. Hii inaonesha tumekuwa tukipiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi,” amesema Prof.Kitila alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na mtangazaji Charles William kuhusu mtazamo wa Watanzania wa kipato cha chini wanaoamini umaskini wao unasababishwa na rushwa na uzembe.

Katika mjadala huo uliojadili mada: “Je, Serikali ya Awamu ya Sita Imeweza Kugusa Maisha ya Watanzania?”, Prof. Kitila amesema ili kuendelea na mapambano hayo, katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025/30 kuna kipengele cha utawala bora chenye lengo la kuimarisha na kudumisha mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi, uzembe na wizi

Amesisitiza kuwa,Serikali ya Awamu ya Sita imejiwekea dhamira ya dhati na imechukua hatua madhubuti katika kudhibiti vitendo vya rushwa na ufisadi, ili kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha Watanzania wote.

Waziri Simbachawene

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene ameendelea kuwahimiza wadau kubuni mikakati na njia mpya za kuzuia na kupambana na rushwa huku akisisitiza kuwa rushwa inadhoofisha utu na heshima ya binadamu.

Ametoa rai hiyo Julai 11, 2025 wakati akifungua Kongamano la Siku ya Mapambano Dhidi ya Rushwa barani Afrika kwa mwaka 2025 iliyoadhimisha kitaifa jijini Dodoma.

Waziri Simbachawene amesema,wakati dunia ikienda na mabadiliko ya teknolojia, kijamii na kisiasa ni vyema wadau wakabuni njia na mikakati mipya ya kuzuia na kupambana na rushwa.

Pia,amesema kuwa, Tanzania inajivunia hatua mbalimbali ilizozichukua katika kupambana na rushwa, ikiwemo kutungwa kwa sheria, kanuni na miongozo inayolenga kukomesha vitendo hivyo.

“Serikali imeongeza bajeti, kutoa vibali vya ajira na kuruhusu ununuzi wa vifaa muhimu kwa taasisi husika ili kuongeza ufanisi wa mapambano haya,” amesema Waziri Simbachawene.

Aidha, ameeleza kuwa, elimu kuhusu madhara ya rushwa imekuwa ikitolewa kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu, ili kujenga jamii yenye uelewa na inayochukia rushwa.

“Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa kila mwaka. Haya ni mafanikio makubwa yanayotokana na jitihada za pamoja za wananchi wote,” ameongeza.

Waziri Simbachawene pia amesema, marekebisho ya sheria yaliyofanyika hivi karibuni yameongeza nguvu zaidi kwa kutambua makosa ya rushwa yanayofanyika katika maeneo mbalimbali ikiwemo upande wa burudani, michezo,chaguzi na mengineyo.

Amesema, kupitia Sheria ya Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007, Taasisi ya Kuzuia na Kupambaba na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) imepewa mamlaka ya kuhakikisha kuwa rushwa inatokomezwa nchini.

"Kwa hiyo tunapaswa kuangalia namna taasisi zetu zinavyohudumia wananchi, kwani huduma bora na haki ni kipimo muhimu cha mafanikio yetu."

Aidha,Mheshimiwa Simbachawene amesema, Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kupambana na Rushwa umeweka misingi ya nchi wanachama kushirikiana katika mafunzo, sheria na mikakati ya kuzuia na kupambana na rushwa kwa pamoja.

Waziri Simbachawene amesema, kupitia mkataba huo, nchi zimewekewa wajibu wa kushughulikia kwa haraka maombi ya vyombo vya dola vinavyohusika na upelelezi, mashitaka, na utoaji wa adhabu kwa watuhumiwa wa makosa ya rushwa na yale yanayohusiana nayo.

TAKUKURU

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Chalamila, amesema rushwa ni kikwazo kikubwa kwa ustawi wa wananchi, kwani inadhalilisha utu wa jamii.

“Kuondoa vitendo vya rushwa kutasaidia kujenga jamii yenye usawa, kuheshimiana na inayowajibika,”amesema Bw.Chalamila.

Amesisitiza kuwa,Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua haki ya kila raia kupata huduma bila upendeleo, hivyo ni wajibu wa kila mtanzania kushiriki katika vita dhidi ya rushwa.

Bw. Chalamila ameongeza kuwa,TAKUKURU inaendelea kubuni mbinu mpya za kushughulikia rushwa ili kuhakikisha huduma zote za kijamii zinatolewa kwa haki bila vitendo vya rushwa.

Mwakilishi wa Bodi ya Ushauri ya Masuala ya Rushwa ya Umoja wa Afrika (AUABC), Bw. Benjamin Kapera ameeleza kuwa,kuendelea kufumbiwa macho kwa vitendo vya rushwa kumesababisha madhara mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuathiri michakato ya uchaguzi barani Afrika.

Vilevile wagonjwa kushindwa kupata matibabu hospitalini, vijana wenye sifa kukosa haki zao, na kudhoofisha mifumo ya utoaji haki na kusisitiza umuhimu wa kuchunguza kwa kina madhara yanayotokana na vitendo vya rushwa.

Kwa mujibu wa Mfuko wa Mo Ibrahim, Afrika inapoteza takribani dola bilioni 128 za Kimarekani kila mwaka kutokana na vitendo vya rushwa, sawa na asilimia 50 ya mapato yake ya kodi na asilimia 25 ya pato la Taifa.

Kufuatia hali hiyo, Kapera amesisitiza kuwa ni muhimu kwa Afrika kuchukua hatua za haraka kushughulikia tatizo la rushwa.

Pia, ametoa wito kwa Serikali za Afrika kuwekeza katika matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ili kuhakikisha uwajibikaji na utoaji wa huduma kwa usawa.

Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema,vitendo rushwa katika jamii havipaswi kufumbiwa macho.

Profesa Kabudi amefafanua kuwa,rushwa inapozidi katika jamii huwa inadhoofisha huduma mbalimbali, hivyo hukosesha watu haki,usawa na kuvuruga utu wa kibinadamu.

Kutokana na changamoto hiyo ambayo rushwa inawapa furaha wachache,amesema kila mmoja wetu anapaswa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa.

Tutimize wajibu

Ikumbukwe kuwa, rushwa ni moja ya vikwazo vikubwa kwa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiutawala katika nchi nyingi duniani.

Rushwa si tu kwamba inasababisha upotevu wa rasilimali za umma, bali pia inadhoofisha mifumo ya haki, inatishia amani na kupunguza imani ya wananchi kwa taasisi za Serikali.

Kwa kiwango chochote, rushwa huathiri moja kwa moja huduma muhimu kama elimu, afya, miundombinu na usalama.

Hivyo,watendaji wanaoweka maslahi binafsi mbele ya maslahi ya wananchi huchelewesha maendeleo, na matokeo yake ni ongezeko la umaskini, ukosefu wa ajira, na kuongezeka kwa pengo kati ya matajiri na maskini.

Zaidi ya hayo, rushwa huwatia hofu wawekezaji wa ndani na wa kimataifa, kwa sababu huonekana kama hatari ya kiuchumi.

Pia huzuia utekelezaji wa sera bora kwa kuwa maamuzi mengi huchukuliwa kwa misingi ya upendeleo badala ya ufanisi na uhalali.

Kwa muktadha huo,tuendelee kuunga mkono jitihada hizi za dhati za Serikali ya Awamu ya Sita katika mapambano dhidi ya rushwa kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwani "Kuzuia rushwa ni jukumu lako na langu:tutimize wajibu wetu”.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news