BoT yashiriki Mkutano wa 48 wa CISNA nchini Botswana

MAUN-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inashiriki Mkutano Mkuu wa 48 na mikutano midogo ya Kamati ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) inayohusiana na Usimamizi wa Bima, Masoko ya Fedha na Taasisi Zisizo za Kibenki (CISNA).
Mkutano huo unaofanyika mjini Maun, nchini Botswana kuanzia Oktoba 5 hadi 10, 2025, unawakutanisha wadau kutoka nchi mbalimbali wanachama wa SADC kujadili masuala ya usimamizi na uimarishaji wa sekta zisizo za kibenki.

Ujumbe wa BoT katika mkutano huo unaongozwa na Naibu Gavana anayeshughulikia Usimamizi na Uthabiti wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Msemo.
Benki Kuu ni mwanachama wa CISNA kutokana na jukumu lake la kusimamia uwekezaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii na taasisi za fedha zisizo za kibenki, zikiwemo zinazotoa huduma ndogo za fedha. BoT ilijiunga rasmi na kamati hiyo baada ya kusaini makubaliano Oktoba 6, 2023.

Mkutano huo ulifunguliwa rasmi Jumanne, Oktoba 7, 2025, na Makamu wa Rais wa Botswana, Mhe. Ndaba Nkosinathi Gaolathe, ambaye aliipongeza CISNA kwa utendaji wake mzuri na kuhimiza kuimarishwa kwa juhudi za kuendeleza uchumi wa ukanda wa SADC.
Alisisitiza umuhimu wa wajumbe wa CISNA kubuni mikakati madhubuti ya kuinua uchumi wa wananchi wa kanda hiyo, huku akipongeza juhudi za kamati hiyo katika kukuza elimu ya kifedha na kuendeleza huduma ndogo za fedha.
CISNA ina jukumu la kuoanisha mifumo ya usimamizi wa huduma za kifedha zinazotolewa na taasisi zisizo za kibenki katika nchi wanachama wa SADC ili kuhakikisha zinazingatia viwango vya kimataifa vinavyowekwa na taasisi husika duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news