SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea rasmi taarifa kutoka Serikali ya Marekani kuhusu uamuzi wa kuiweka Tanzania na baadhi ya nchi zingine za Afrika, kwenye orodha ya nchi ambazo raia wake watatakiwa kuweka dhamana ya viza (visa bond) ili kuingia nchini Marekani kwa ajili ya shughuli za biashara (viza za B-1) au utalii (viza za B-2), kuanzia tarehe 23 Oktoba 2025.
Taarifa ya leo Oktoba 8, 2025 iliyotolewa na Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa imeeleza kuwa uamuzi huo umefikiwa wakati majadiliano kuhusu masuala ya uhamiaji na uhamaji yakiendelea baina ya Tanzania na Marekani.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa pamoja na hatua hiyo ya Marekani, Serikali ya Tanzania itaendelea na majadiliano hayo na Serikali ya Marekani kwa njia za kidiplomasia ili kutafuta suluhisho lenye kuzingatia usawa, heshima, na maslahi ya pande zote mbili kwa kuzingatia uhusiano mzuri uliodumu kwa zaidi ya miongo minne (4).
“Kadhalika, Serikali ya Tanzania inasisitiza kwamba uhusiano wake na Marekani umejengwa katika misingi ya urafiki, ushirikiano, na kuheshimiana kwa muda mrefu, na hivyo hatua hii haitabadilisha dhamira ya Tanzania ya kuendeleza uhusiano mzuri na nchi hiyo kwa manufaa kwa pande zote.”
“Kwa sasa, wananchi wanaombwa kuendelea kufuata taratibu za kawaida za maombi ya viza kupitia Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania na popote ambapo Mtanzania muombaji wa viza husika atakuwepo. Serikali itatoa taarifa zaidi kuhusu suala hili pindi mazungumzo yanayoendelea yatakapofikia hatua nyingine;
