NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeendelea kufumua na kusambaratisha mitandao hatari ya dawa za kulevya nchini, huku operesheni zake zikiendelea kuleta matokeo chanya katika kulinda afya ya jamii na usalama wa taifa.
Katika kipindi cha mwezi Septemba na Oktoba, 2025 mamlaka hiyo imekamata jumla ya kilo 10,763.94 za dawa za kulevya aina mbalimbali.
Sambamba na kilo 6,007 zikiwemo lita 153 za kemikali bashirifu, katika operesheni maalum zilizofanyika katika maeneo mbalimbali nchini.
“Dawa za kulevya si tu zinaharibu afya za watumiaji, bali zinatishia usalama wa taifa, uchumi na mustakabali wa kizazi kijacho. Hatutasita kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayehusishwa."
Hayo yamebainishwa leo Oktoba 21,2025 na Kamishna Jenerali wa DCEA,Aretas Lyimo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Kamisha Jenerali Lyimo amesema,mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano thabiti kati ya mamlaka hiyo na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya nchini.
Amesema,katika operesheni moja iliyofanyika katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam, mamlaka ilibaini mbinu mpya ya kusafirisha dawa za kulevya kimataifa, ambapo kilo 40.32 za mirungi zilizokaushwa na kufungwa kwenye paketi 80 zenye maandishi ya Dry Basil Leaves zilinaswa zikiwa tayari kusafirishwa kuelekea nchini Canada na Italia kupitia kampuni za usafirishaji.
Watuhumiwa wawili waliokamatwa katika tukio hilo ni Yusuphu S.Kibaha (35) na Mohamed H. Ramadhan (41),ambapo uchunguzi wa awali umebaini kuwa dawa hizo ziliingizwa nchini kwa njia zisizo halali kutoka nchi jirani.
“Uchunguzi wetu umebaini uwepo wa mtandao wa kusafirisha mirungi unaohusisha baadhi ya waendesha bodaboda na mawakala wa kampuni za usafirishaji, jambo linalohatarisha usalama wa taifa na sifa ya nchi kimataifa,” ameeleza Kamishna Jenerali Lyimo huku akitoa onyo kali kwa makundi hayo.
Katika tukio lingine lililoshangaza wengi, operesheni maalum katika eneo la Mlalakuwa, Kinondoni jijini Dar es Salaam iligundua kundi la vijana waliokuwa wakitengeneza biskuti za bangi kwa ajili ya sherehe ya kujirusha (house party) ya wanafunzi wa vyuo vikuu.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Bright A. Malisa, Humphrey G. Safari, Novatus A. Kileo, na Chriss P. Mandoza wote wakiwa na umri wa miaka 26.
Katika tukio hilo, walikutwa na biskuti 140 za bangi, puli nane, na pakiti tisa za bangi zenye uzito wa kilo 2.858.
“Matumizi ya dawa hizi kwa kisingizio cha starehe miongoni mwa vijana ni tishio kwa afya na ustawi wa taifa. Tunatoa wito kwa vijana kujiepusha na makundi yenye tabia potofu na kutumia muda wao kwa shughuli za maendeleo,”amesisitiza Kamishna Jenerali Lyimo.
Pia, amesema mamlaka inafanya uchunguzi maalum kuhusu matumizi ya bangi katika bidhaa mbalimbali ikiwemo vyakula, vinywaji, vipodozi na sigara za kielektroniki (vapes), ambapo baadhi ya bidhaa zimebainika kuwa na viambata vya dawa hizo.
Katika mikoa mbalimbali, DCEA kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, ilikamata kilo 9,164.92 za bangi, kilo 1,555.46 za mirungi, gramu 367 za skanka, na gramu 7.498 za heroin, pamoja na kuteketeza ekari 11.5 za mashamba ya bangi.
Kamishna Jenerali Lyimo ametoa wito kwa waendesha bodaboda, mawakala wa usafirishaji na wamiliki wa kampuni kuwa makini na mizigo wanayosafirisha, akisisitiza kuwa yeyote atakayebainika kushiriki au kusaidia uhalifu wa aina hiyo, hatasazwa na mkono wa sheria.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)
