NA GODFREY NNKO
JUMUIYA ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imewahimiza wapiga kura wote waliosajiliwa nchini Tanzania kujitokeza kwa wingi ili kutumia haki yao ya kidemokrasia na kikatiba ya kupiga kura Oktoba 29,2025.
Wito huo umetolewa leo Oktoba 21,2025 na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC (SEOM) katika Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Spika mstaafu wa Bunge la Malawi,Mheshimiwa Richard Msowoya wakati akizindua misheni hiyo jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Msowoya amezindua misheni hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC na Rais wa Jamhuri ya Malawi, Profesa Arthur Peter Mutharika.
Aidha,misheni hiyo imetoa wito kwa wadau wote kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu huo unafanyika kwa amani, uhuru, haki, uwazi na kwa njia ya kuaminika.
"Tunatarajia mchakato wa uchaguzi utazingatia misingi ya kidemokrasia iliyoainishwa katika Mkataba wa SADC, Itifaki ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama, pamoja na Mwongozo ulioboreshwa wa SADC kuhusu Uchaguzi."
Amesema, ujumbe wa SEOM nchini Tanzania unajumuisha jumla ya watu 80 kutoka katika nchi 10 wanachama wa SADC, ambazo ni Ufalme wa Eswatini, Ufalme wa Lesotho, Jamhuri ya Botswana, Malawi, Msumbiji, Namibia, Zimbabwe, Zambia, Shelisheli na Afrika Kusini.
"Kwa kuzingatia muda na rasilimali zilizopo, ujumbe huu hautaweza kukutana na vyama vyote vya siasa nchini.
"Hata hivyo, waangalizi wetu watapelekwa katika mikoa 27 kati ya 31 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo kusaidia juhudi za makao makuu ya ujumbe huu kufuatilia mchakato mzima wa uchaguzi,"amesisitiza.
Vilevile amesema kuwa, kutokana na changamoto za uwezo, SEOM haitapeleka waangalizi katika mikoa ya Mtwara, Singida, Tabora na Tanga.
Mheshimiwa Msowoya amesema,waangalizi hao watafanya kazi katika vipindi vyote vya uchaguzi vya kabla ya uchaguzi, siku ya kupiga kura na baada ya uchaguzi.
Amesema, vipindi hivyo vinajumuisha ufuatiliaji wa kampeni, zoezi la upigaji kura na kuhesabu kura Tanzania Bara na Zanzibar.
