MTWARA-Katika kuhakikisha lango la kusini haligeuki kuwa njia ya usafirishaji wa dawa za kulevya, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeendesha mafunzo maalum kwa watumishi wa Uwanja wa Ndege wa Mtwara, yakilenga kuimarisha uelewa na ulinzi dhidi ya biashara haramu ya dawa hizo.
Mafunzo hayo yamelenga kuwakumbusha watumishi hao juu ya ukubwa wa tatizo la dawa za kulevya nchini, pamoja na mbinu mpya zinazotumiwa kusafirisha dawa hizo kupitia viwanja vya ndege.
Katika mafunzo hayo, watumishi walipata nafasi ya kuona sampuli mbalimbali za dawa za kulevya, namna zinavyofungwa pamoja na kujifunza kuhusu namna ya kumtambua mtumiaji.
Vilevile sababu za matumizi,madhara na tiba, jinsi ya kujiepusha na matumizi na utekelezaji wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.
Watumishi hao walisisitizwa kuendelea kushirikiana na DCEA katika kudhibiti biashara na matumizi ya dawa za kulevya kwa ajili ya usalama wa taifa letu.
Mafunzo haya yamekuja wakati ambapo dunia inakabiliwa na ongezeko la usafirishaji wa dawa za kulevya kwa njia zisizotarajiwa, hali inayoilazimu Tanzania kuimarisha mifumo yake ya ulinzi kuanzia viwanja vya ndege,mipakani,majini na katika jamii.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)





