NA LWAGA MWAMBANDE
REJEA neno la Mungu katika Biblia Takatifu kitabu cha Kumbukumbu la Torati 4:23-24..."Jihadharini, msilisahau agano la Bwana, Mungu wenu, alilofanya pamoja nanyi; wala msijifanyie sanamu ya mfano wa kitu chochote alichokataza Bwana, Mungu wenu, kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, ni moto ulao, Mungu mwenye wivu.”
Ukitafakari neno la Mungu, utabaini kuwa "Mungu ni moto ulao” si kauli ya kitisho tu, bali ni onyo la upendo kwa mwanadamu amtambue Mungu kama mwenye haki, mtakatifu na mwenye uwezo wa kuokoa na pia kuangamiza.
Kauli hii inatufundisha kuwa, maisha ya Mkristo yanapaswa kuwa ya kumcha Mungu, kuishi kwa utakatifu na kukwepa kila namna ya uovu.
Aidha, kauli hii inahimiza umuhimu wa kuishi maisha ya toba na kujitakasa kila siku, kwa kuwa Mungu hashirikiani na dhambi. Kama moto, Mungu husafisha, hutoa nuru, lakini pia huangamiza kila kilicho kiovu.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anakumbushia kuwa, tunapaswa kukumbuka kwamba, Mungu si wa kubezwa,kwani licha ya kusafisha kwa moto, anaweza pia kuangamiza kwa moto, hivyo tumche kwa hofu na kwa heshima.Endelea;
1. Ufalme tunapokea, ule usotetemeshwa,
Vema tukaendelea, nasi kutotetemeshwa,
Neema kiendelea, na Mungu kuadhimishwa,
Kwa maana Mungu wetu, yeye ni moto ulao.
2. Sisi tunatetemesha, hapa tulipofikishwa,
Uwepo wetu watisha, wabaya wadhoofishwa,
Tuzidi jiimarisha, na Neno tusijechoshwa,
Kwa maana Mungu wetu, Yeye ni moto ulao.
3. Tutakiwacho kufanya, kwa vazi tulilovishwa,
Ibada njema kufanya, ya Mungu kupendezeshwa,
Tusifu anayofanya, kufanya tukawandishwa,
Kwa maana Mungu wetu, Yeye ni moto ulao.
4. Kwa Mungu tunyenyekee, kwa vile tulivyovushwa,
Na tena tuchekelee, hapa tulipofikishwa,
Tena tusherehekee, kwake kushatayarishwa,
Kwa maana Mungu wetu, Yeye ni moto ulao.
5. Kwa Mungu tuko enzini, hatuwezi kutoweshwa,
Vile Mungu wa mbinguni, alipo hawezi shushwa,
Hivyo tuwe na imani, ngámbo take tumevushwa,
Kwa maana Mungu wetu, Yeye ni moto ulao.
6. Nafasi tuliyopewa, kule kutotetemeshwa,
Ni vema ikatumiwa, kwao wanaopofushwa,
Neno waweze ambiwa, uovu uweze furushwa,
Kwa maana Mungu wetu, Yeye ni moto ulao.
7. Mwovu hata akipinga, yale wanayofundishwa,
Hata silaha kuchonga, ili tuweze dondoshwa,
Muumba atamtwanga, ndivyo atawajibishwa,
Kwa maana Mungu wetu, Yeye ni moto ulao.
8. Tunene kwa ujasiri, injili tulofundishwa,
Na wala tusisubiri, na mtu kuamrishwa,
Kwa wote wenye kiburi, chote kiweze komeshwa,
Kwa maana Mungu wetu, Yeye ni moto ulao.
9. Mungu ni moto ulao, kwa Neno tunafundishwa,
Kwake hakuna makao, wachafu wasosafishwa,
Tusiishi kama wao, tusijekutetemeshwa,
Kwa Maana Mungu wetu, Yeye ni moto ulao.
10. Ufalme wake Muumba, ule usotetemeshwa,
Ni mfumo aloumba, ule usiokomeshwa,
Yeye akiwa ni Mwamba, kwake yetu yakinyoshwa,
Kwa Maana Mungu wetu, Yeye ni moto ulao.
11. Na tuishi kwa amani, siyo wa kutetemeshwa,
Hata kutokee nini, Mungu wa kuadhimishwa,
Duniani na mbinguni, kwake vyote vyakomeshwa,
Kwa Maana Mungu wetu, yeye ni moto ulao.
(Waebrania 12:28-29)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
