DAR-Klabu ya Simba SC imemtambulisha rasmi Dimitar Pentev, raia wa Bulgaria, kuwa Kocha Mkuu na Meneja mpya wa klabu hiyo ya jijini Dar es Salaam.
Ujio wa Pentev unakuja kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Fadlu Davids, ambaye alijiunga na klabu ya Raja Casablanca ya Morocco hivi karibuni.
Kabla ya kujiunga na Simba, Pentev alikuwa Kocha Mkuu wa Gaborone United ya nchini Botswana, ambako alionekana kufanya kazi nzuri na kuacha alama katika soka la ukanda huo.
Uzoefu wake katika soka la Afrika unatajwa kuwa moja ya sababu zilizomvutia Simba SC kumleta Msimbazi.
Mashabiki wa Simba na wadau wa soka kwa ujumla wanafuatilia kwa karibu kuona mwelekeo mpya chini ya Pentev, huku wengi wakitarajia atakuja kuongeza ushindani na kuleta mafanikio zaidi kwa klabu hiyo kubwa nchini.
