Dkt.Mwinyi aahidi maendeleo endelevu na ustawi bora wa wananchi Zanzibar

ZANZIBAR-Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi maendeleo endelevu katika sekta mbalimbali za uchumi na kijamii.
Dkt.Mwinyi ameyasema hayo katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo Oktoba 18,2025 katika Uwanja wa Michezo wa Kihinani uliopo Mkoa wa Mjini Magharibi.

Katika mkutano huo,Dkt.Mwinyi alikutana na makundi mbalimbali ya wananchi wakiwemo wajasiriamali, waendesha bodaboda na bajaji, wajane, wavuvi na wakulima.
Amesema, serikali itaendelea kujenga masoko katika kila wilaya na mkoa ili kuwezesha wajasiriamali kufanya biashara zao kwa ufanisi katika mazingira salama na ya kisasa.

Pia, Dkt.Mwinyi ameahidi kutoa mafunzo ya biashara na alama za ubora kwa wajasiriamali ili bidhaa zao ziweze kushindana katika masoko ya kimataifa.

Vilevile, atahakikisha tozo za masoko zinapunguzwa na mikopo nafuu itatolewa kwa wajasiriamali waliojiandikisha rasmi.

Katika sekta ya kilimo,Dkt.Mwinyi ameahidi kuimarisha skimu za umwagiliaji, kusambaza pembejeo na mbolea kwa bei nafuu pamoja na kutoa mafunzo na vifaa vitakavyoongeza uzalishaji wa chakula.

Sekta ya uvuvi pia, amesema itapewa mkazo kwa ujenzi wa masoko ya kisasa, madiko na viwanda vya kusafisha samaki, hasa eneo la Fungu Refu, pamoja na gati jipya Kihinani.
Dkt. Mwinyi pia ametoa ahadi za kuendelea kusaidia wajane kupitia mikopo isiyo na riba na mafunzo ya kiuchumi, pamoja na kuchukua hatua kali dhidi ya wazazi wanaotelekeza watoto wao.

Amewaomba wananchi wa Zanzibar kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Oktoba 29,2025 ambapo pia itakuwa siku ya mapumziko.

“Mchango wa kila mmoja ni muhimu katika kuijenga Zanzibar yenye uchumi imara, jamii yenye ustawi na mazingira bora kwa maendeleo ya wote,”amesema Dkt.Mwinyi huku akiendelea kusisitiza kila mmoja ana wajibu wa kudumisha amani,umoja na mshikamano nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news