ZANZIBAR-Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo Oktoba 16,2025 amekutana na wafanyabiashara pamoja na wajasiriamali wa Soko la Darajani kwa lengo la kusikiliza changamoto zao na kueleza mikakati ya Serikali katika kuimarisha mazingira ya biashara visiwani humo.
Katika mkutano huo, Dkt.Mwinyi ameeleza kuridhishwa na mwenendo wa biashara katika eneo la Darajani, akisema Serikali imekuwa ikitekeleza hatua mbalimbali za kuboresha mazingira ya wafanyabiashara kwa lengo la kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.
“Tumeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha mazingira ya kufanya biashara yanakuwa bora zaidi. Maendeleo haya tunayoyaona leo Darajani ni matokeo ya juhudi za pamoja kati ya Serikali na wafanyabiashara,” amesema Dkt.Mwinyi.
Akitangaza mipango ya Serikali, Dkt. Mwinyi amesema maegesho ya kisasa yanatarajiwa kujengwa katika eneo la Malindi ili kuondoa msongamano na kuepuka uegeshaji holela wa magari.
Aidha, ameeleza kuwa, utekelezaji wa mradi mkubwa wa BIG Z utahusisha ujenzi wa maduka pembezoni mwa barabara, hatua itakayoongeza haiba ya mji wa Zanzibar.
Vilevile, Dkt. Mwinyi ametangaza mpango wa kupanua barabara ya Malindi hadi Mnazi Mmoja kuwa ya njia nne, sambamba na ujenzi wa maegesho mapya katika eneo la Malindi, hatua inayolenga kurahisisha usafiri na kuboresha mandhari ya jiji.
Kuhusu uwezeshaji wa wafanyabiashara, Dkt. Mwinyi amesema, Serikali katika awamu ijayo itaongeza fungu la fedha kwa ajili ya mikopo, hususan kwa wale waliokopa na kurejesha kwa wakati, ili kuwaongezea mitaji na uwezo wa kiuchumi.
Akigusia suala la kodi, Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na CCM kujadiliana namna bora ya kupunguza changamoto za kikodi kwa wafanyabiashara. Pia aliiagiza Mamlaka ya Umeme Zanzibar (ZECO) kusimika transfoma mpya katika eneo la Darajani ili kutatua tatizo la umeme.
“Nawaomba wananchi na wafanyabiashara waendelee kuniunga mkono kwa kura nyingi katika uchaguzi ujao, ili tuweze kuendeleza juhudi hizi za maendeleo, kudumisha amani, umoja na ustawi wa Zanzibar."
Wafanyabiashara wa Darajani wamemshukuru Dkt. Mwinyi kwa jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara, kurejesha kituo cha daladala na kuimarisha bustani, hatua ambazo zimesaidia kuongeza wateja na kuufanya mtaa huo kuwa hai zaidi.










.jpg)










