Dokta Jane Goodall,kamaliza ngwe yake

NA LWAGA MWAMBANDE

OKTOBA 1,2025 ilikuwa ni siku ngumu kwa watafiti wa wanyama na wadau wa mazingira duniani, baada ya kupata taarifa ya kifo cha Dkt.Valerie Jane Morris-Goodall maarufu kama
Dkt.Jane Goodall.
Mtafiti huyo mashuhuri wa wanyama, hasa sokwe na pia mwanaharakati wa mazingira kutoka Uingereza,anajulikana zaidi kwa utafiti wake wa muda mrefu juu ya tabia za sokwe kwenye Hifadhi ya Taifa ya Gombe inayopatikana mkoani Kigoma.

Licha ya udogo wake,Hifadhi ya Taifa ya Gombe inafahamika kuwa na sokwe wengi na imehifadhiwa kwa ajili ya wanyama hao.

Dkt.Jane Goodall ambaye alizaliwa Aprili 3, 1934 huko London nchini Uingereza,alijulikana duniani kwa kazi yake ya kipekee ya utafiti wa sokwe katika hifadhi hiyo.

Mama huyo alianza kazi hiyo mwaka 1960 ambapo aligundua tabia mpya kwa sokwe kama kutumia vifaa (zana), kabla ya hapo ilidhaniwa kuwa ni binadamu tu wenye uwezo huo.

Pia, aligundua tabia ya kijamii na kihemko miongoni mwa sokwe, kama vile huruma, uhasama na hata vita baina ya makundi.

Mbali na hayo, mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anabainisha kuwa, Dkt.Jane Goodall ana mengi ambayo kizazi cha sasa na kijacho kinaweza kujifunza kwa ustawi bora wa mazingira, wanyama na jamii hususani kupitia vitabu vyake na taasisi ya Jane Goodall Institute. Endelea;

1. Dokta Jane Goodall, ni nani hakumjua,
Jinsi alikuwa mali, uhifadhi kuibua,
Wala tusiende mbali, hifadhi Gombe twajua,
Ila sasa hatunaye, kamaliza ngwe yake.

2. Habari yasikitisha, sote tuliomjua,
Alivyojishughulisha, uhifadhi kuinua,
Wanyama kijifundisha, hata vema kuwajua,
Ila sasa hatunaye, kamaliza ngwe yake.

3. Uhifadhi kule Gombe, sokwe hao twawajua,
Na mbuga yetu tutambe, kazi yake kutambua,
Kweli bora tumuimbe, kazi yake alijua,
Ila sasa hatunaye, kamaliza ngwe yake.

4. Miaka sitina mbili, muda aliochukua,
Kufanya kazi ghali, ya wanyama kuwajua,
Lipenda wanyama kweli, tabiazo lizijua,
Ila sasa hatunaye, kamaliza ngwe yake.

5. Mzee mekula siku, miaka ametanua,
Tisini na moja mtu, maisha aliyajua,
Lijali dunia yetu, mazingira kutoua,
Ila sasa hatunaye, kamaliza ngwe yake.

6. Dunia inatumeza, kama inatuanua,
Malengo tukitimiza, yale Mungu anajua,
Kila mtu bora waza, ni nani anakujua,
Ila sasa hatunaye, kamaliza ngwe yake.

7. Hapa kwetu Tanzania, Goodall tulimjua,
Na yeye kwa yake nia, nchi yetu liijua.
Muda mwingi litumia, sokwe azidi wajua,
Ila sasa hatunaye, kamaliza ngwe yake.

8. Jane Goodall twajua, nchi aliinua,
Uhifadhi livyojua, hatua alichukua,
Si wanyama kuwaua, kutunza tuweze jua,
Ila sasa hatunaye, kamaliza ngwe yake.

9. Atabaki akumbukwa, yale kwake tunajua,
Japokuwa atazikwa, vyakutosha kakamua,
Kumbukumbu itawekwa, bila mtu kutangua,
Ila sasa hatunaye, kamaliza ngwe yake.

10. Pole ndugu na jamaa, wote waliomjua,
Wale naye walikaa, mambo mengi kutatua,
Roho yake ishapaa, aliko mwenyewe ajua,
Ila sasa hatunaye, kamaliza ngwe yake.

11. Sokwe wangekuwa watu, yalotokea kujua,
Ingekuwa kilio tu, jinsi alivyowajua,
Sasa imebaki kwetu, mbuga kuzidi inua,
Ila sasa hatunaye, kamaliza ngwe yake..

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news