DAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa viongozi wapya katika taasisi zinazoshughulikia usafiri wa mabasi yaendayo haraka nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, uteuzi huo unawahusisha viongozi wawili:
(i) Bw. Said Habibu Tunda ameteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART). Anachukua nafasi ya Dkt. Athumani Kihamia ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
(ii) Bw. Pius Andrew Ng’ingo ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Bw. Waziri Kindamba, ambaye uteuzi wake pia umetenguliwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uteuzi huo unaanza mara moja, ambapo hatua hii inaashiria dhamira ya Serikali katika kuboresha utoaji wa huduma za usafiri wa umma kupitia mfumo wa mabasi yaendayo haraka, hasa katika Jiji la Dar es Salaam.
Mwezi Machi,2024 Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alimteua Waziri Kindamba kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART).
Kindamba kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga na alichukua nafasi ya Gilliard Wilson Ngewe ambaye alipangiwa kazi nyingine.
Aidha, Januari, mwaka 2024 Rais Dkt.Samia alimteua Dkt. Athuman Kihamia kuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART). Dkt. Kihamia aliwahi kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha.
Dkt. Kihamia alichukua nafasi ya Dkt. Edwin P. Mhede ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na kupangiwa kazi nyingine.
.jpeg)