WASHINGTON-Nchi 14 za Afrika za Kundi la Kwanza, wanachama wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), zimekubaliana kuimarisha mikakati ya kukuza uwekezaji wa sekta binafsi na kuongeza mapato ya ndani ili kukabiliana na kupungua kwa mikopo na misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Makubaliano hayo yalifikiwa katika Mkutano wa 52 wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika (Africa Group 1 Constituency Policy Dialogue), uliofanyika pembezoni mwa Mikutano ya Mwaka ya IMF na Benki ya Dunia jijini Washington D.C nchini Marekani.
Tanzania iliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba, pamoja na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba.
Dkt.Mwamba alisema kuwa,nchi wanachama zimeazimia kuimarisha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya maendeleo ya wananchi, huku Tanzania ikitajwa kufanya vizuri katika kuongeza uwazi wa bajeti na ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Aidha, alibainisha kuwa Tanzania inaendelea kutekeleza sera za fedha zinazolenga ukuaji jumuishi na uthabiti wa uchumi kupitia mageuzi ya mifumo ya kodi, matumizi ya teknolojia za kidijitali, na uboreshaji wa vyanzo vya mapato vya serikali za mitaa.
Kuhusu njia ya kusonga mbele kama Ukanda, alisema kuwa mipango inayoungwa mkono na IMF inapaswa kuendelea kuwa kichocheo muhimu cha kuhamasisha upatikanaji wa fedha zenye masharti nafuu na zenye kuwezesha nchi za Afrika kuhimili mabadiliko ya tabianchi.


