WASHINGTON-Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt.Yamungu Kayandabila ameshiriki kikao cha Taasisi ya Usimamizi wa Uchumi na Fedha katika Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (MEFMI), kilichojadili fursa na changamoto za matumizi ya Akili Bandia (AI) katika uzalishaji wa uchumi.
Kikao hicho kimefanyika kando ya mikutano ya mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia inayoendelea Washington D.C nchini Marekani.
Majadiliano hayo yalijikita katika kuangazia namna AI inavyoweza kurahisisha ukusanyaji wa mapato, kuhifadhi na kuchambua data kwa ajili ya maamuzi ya kisera, pamoja na kuboresha ugawaji wa rasilimali fedha na usimamizi wa mifumo ya utoaji huduma za fedha katika nchi hizo.
Hata hivyo, baadhi ya changamoto zinazoikabili teknolojia ya AI katika utekelezaji wake kwa nchi wanachama ni pamoja na upungufu wa wataalamu, uhaba wa miundombinu imara, na changamoto za usalama wa taarifa.Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika zimeshauriwa kuwekeza katika teknolojia ya AI ili ziweze kwenda sambamba na maendeleo ya nchi zilizoendelea.
