NA GODFREY NNKO
MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Jaji Mshibe Ali Bakari amewataka washindi wa Tuzo za Habari za Hali ya Hewa kwa mwaka 2025 kuhakikisha kuwa wanazidisha juhudi badala ya kubweteka na mafanikio waliyoyapata.
Jaji Mshibe ameyasema hayo Oktoba 16,2025 wakati akiwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji tuzo za wanahabari bora wa habari za hali ya hewa kwa mwaka 2025 iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) jijini Dar es Salaam.
"Washindi wote mliopata tuzo za habari za hali ya hewa 2025 nawasihi msibweteke, sababu nimeona washindi wengi waliopata tuzo mwaka jana hawapo mwaka huu. Inapaswa ikiwa umepata tuzo mwaka huu basi mwaka unaofuata ufanye vizuri zaidi.
"Endeleeni kujiamini na kuandika taarifa sahihi kwa maslahi ya kujenga Tanzania, hivyo tunzeni tuzo hizi kwani ni alama kubwa katika kazi zenu,"amesisitiza Jaji Mshibe.
Katika hafla hiyo, washindi wa tuzo walitangazwa katika makundi mbalimbali ambapo mwanahabari Lisungu Kambona kutoka ZCTV aliibuka mshindi katika kipengele cha runinga na redio.
Aidha,Penina Malundo wa gazeti la Majira alishinda upande wa magazeti,Amour Khamis Ali wa Assalam FM kutoka Zanzibar alinyakua tuzo ya mwandishi bora kutoka visiwani Zanzibar.
Naye Juma Issihaka kutoka Mwananchi Digital alishinda katika kipengele cha Mitandao ya Kijamii ikiwa tuzo hizo kwa mwaka huu zimeboreshwa zaidi ambapo, pia kulikuwa na mshindi wa pili na wa tatu.
Jaji Mshibe ameipongeza TMA kwa kuendeleza utaratibu wa utoaji wa tuzo hizo ambazo, kwa mujibu wake, zimekuwa na mchango mkubwa katika kuhamasisha waandishi wa habari kuandika habari za hali ya hewa kwa usahihi na taaluma.
"Tuzo hizi ni chachu ya uboreshaji wa mawasiliano ya hali ya hewa kwa jamii. Naipongeza TMA kwa kuendelea kutoa motisha kwa wanahabari ambao wana mchango mkubwa katika kuielimisha jamii," aliongeza Jaji Mshibe.
Tuzo hizi zimekuwa zikitolewa kila mwaka tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019, na mwaka huu zimetolewa kwa mara ya sita.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA ) Dkt.Ladislaus Chang’a amesema,mamlaka hiyo inaendelea kutambua mchango mkubwa wa wanahabari na kuimarisha mahusiano hayo kwa kuendelea kutoa motisha mbalimbali kwa wanahabari ikiwemo kutoa mafunzo ya mara kwa mara hususani kipindi cha maandalizi ya utabiri wa mvua za misimu.
Pia,TMA iliendelea kuwataka wanahabari kuzingatia taarifa sahihi za hali ya hewa kutokaba na muhimu wake kwa maisha ya kila siku na kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Ikumbukwe kuwa,hali ya hewa huathiri shughuli nyingi kama kilimo, usafiri, afya, na hata usalama wa watu.
Kupitia taarifa hizi, watu huweza kujiandaa mapema kwa hali mbaya ya hewa kama mafuriko, upepo mkali, au ukame.
Aidha,kwa wakulima, taarifa sahihi huwasaidia kujua wakati mzuri wa kupanda au kuvuna, hivyo kuongeza uzalishaji wa chakula.
Katika usafiri wa anga, majini na barabara, taarifa za hali ya hewa husaidia kuepusha ajali na kuchelewesha safari kwa usalama wa abiria.
Pia, sekta ya afya hutumia taarifa hizi kukabiliana na magonjwa yanayochochewa na mabadiliko ya hali ya hewa kama vile malaria au magonjwa ya mapafu.
Kwa ujumla, taarifa sahihi za hali ya hewa huokoa maisha, huongeza uzalishaji, na kusaidia kupanga maendeleo kwa usahihi.
Hata hivyo,kabla ya hafla hiyo, waandishi wa habari walishiriki katika warsha maalum kuhusu mwelekeo wa mvua za msimu wa Novemba 2025 hadi Aprili,2026.
Tags
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Tuzo za Hali ya Hewa Tanzania
Tuzo za TMA
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania

