Msimu wa mvua wa tahadhari,TMA yawataka wadau kujipanga mapema

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa mvua za msimu kwa kipindi cha Novemba 2025 hadi Aprili 2026, ikitoa ujumbe mzito kwa jamii na wadau mbalimbali nchini kuchukua hatua za tahadhari na kupanga kwa makini shughuli zao, hasa katika sekta zinazotegemea mvua kama kilimo, mifugo,afya na miundombinu.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Sayansi la Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a ameyabainisha hayo leo Oktoba 17,2025 jijini Dar es Salaam wakati akitoa utabiri huo mbele ya waandishi wa habari.

Amesema,msimu huu utatawaliwa na mvua za chini ya wastani hadi wastani, hali inayoweza kuathiri kwa kiasi kikubwa maisha na uchumi wa wananchi.

Maeneo yanayopata msimu mmoja, Dkt.Chang’a ameyataja kuwa ni Kanda ya Magharibi inayojumuisha mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Kanda ya Kati inayojumuisha mikoa ya Singida na Dodoma.

Pia,kuna Nyanda za Juu Kusini Magharibi inayojumuisha mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa, Iringa, Njombe na Kusini mwa Nchi inayojumisha Mkoa wa Ruvuma, na Pwani ya Kusini inayojumuisha Lindi na Mtwara.

Dkt.Chang’a amesema,Kusini mwa Morogoro, mvua zinatarajiwa kuanza kati ya Oktoba hadi Desemba 2025, na kuisha mwishoni mwa Aprili hadi Mei, 2026.

Hata hivyo, utabiri unaonesha kuwa kutakuwa na vipindi virefu vya ukavu na mvua zitanyesha kwa mtawanyiko usioridhisha, hali inayoweza kusababisha upungufu wa maji na chakula.

“Ongezeko la mvua linatarajiwa tu katika nusu ya pili ya msimu, yaani kuanzia Februari hadi Aprili 2026,”amesema Dkt.Chang’a.

Kutokana na upungufu wa mvua, Dkt.Chang’a amesema,uhaba wa maji safi kwa matumizi ya nyumbani unatarajiwa kuongezeka.

Mamlaka za mitaa zimeshauriwa kuimarisha mifumo ya usambazaji maji na kuelimisha wananchi kuhusu matumizi bora ya maji.

Pia,wakulima na wafugaji wanashauriwa kushauriana na wataalamu wa kilimo na mifugo ili kubadilisha aina ya mazao na mbinu za kilimo kulingana na upatikanaji wa mvua,na upungufu wa malisho unatarajiwa kuathiri ufugaji.

Katika maeneo yatakayokumbwa na uhaba wa mvua, wananchi watalazimika kutumia maji yasiyo salama, hivyo kuongeza hatari ya milipuko ya magonjwa ya tumbo.

Dkt.Chang’a amesema,Wizara ya Afya na mamlaka husika zinapaswa kuweka mikakati madhubuti ya usafi wa mazingira na upatikanaji wa dawa.

Vilevile,kampuni zinazotegemea malighafi za kilimo, miti au mifugo zinaweza kuathiriwa kwa kiasi kikubwa.

Hii inaweza kupelekea kupanda kwa gharama za uzalishaji na kupungua kwa ubora wa bidhaa.

Taasisi za kifedha, benki na bima zinahimizwa kusaidia kwa kutoa huduma maalum kwa biashara zilizo hatarini.

Dkt.Chang’a amesema,vipindi vya mvua kubwa vinaweza kusababisha mafuriko ya kushtukiza, maporomoko ya ardhi na uharibifu wa miundombinu.

Kutokana na hali hiyo,Kamati za Maafa kuanzia kijiji hadi taifa zimeshauriwa kujiandaa na mikakati ya kukabiliana na hali hiyo, ikiwa ni pamoja na uelimishaji na uhifadhi wa chakula.

Wakati huo huo,TMA imesisitiza kuwa ni muhimu kwa vyombo vya habari kushirikiana na wataalamu wa hali ya hewa katika kutoa taarifa sahihi na kwa wakati.

Aidha, jamii imehimizwa kutumia taarifa rasmi kutoka TMA tu, kama inavyoelekezwa na Sheria ya TMA Na. 2 ya mwaka 2019.

“Ni kosa kisheria kusambaza taarifa za hali ya hewa kutoka vyanzo visivyo rasmi,”ameongeza Dkt.Chang’a.

TMA itaendelea kutoa taarifa za mwenendo wa hali ya hewa, hivyo wadau wanahimizwa kufuatilia kwa ukaribu na kuwasiliana moja kwa moja na Mamlaka kwa taarifa mahsusi kulingana na mahitaji yao.

Msimu huu unahitaji maandalizi ya pamoja na ushirikiano wa karibu baina ya Serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia na wananchi wote.

Kwa kuzingatia utabiri huu, kila sekta ina nafasi ya kujiandaa mapema, ili kupunguza athari na kuhakikisha uendelevu wa shughuli za kijamii na kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news