NA DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imethibitisha kuwa kilichokuwa Kimbunga Chenge kimepoteza nguvu zake na kusambaratika kabisa kabla ya kufika katika ukanda wa pwani ya Tanzania, licha ya kusababisha vipindi vya mvua katika baadhi ya maeneo ya pwani.
Kwa mujibu wa taarifa ya TMA, mabaki ya kimbunga hicho yamesababisha mvua na mawingu kuenea katika mikoa ya Lindi, Pwani, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, ambapo baadhi ya maeneo yameripoti mvua nyepesi hadi za wastani.Aidha,taarifa hiyo imeeleza kuwa, hadi kufikia saa 12 jioni ya jana, kituo cha hali ya hewa cha Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (Dar es Salaam) kilirekodi mvua ya milimita 9.1 kwa kipindi cha saa tisa, huku kituo cha Bandari ya Dar es Salaam kikiripoti mvua ya milimita 3.5 katika kipindi hicho hicho.
TMA imefafanua kuwa,uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha mabaki ya kimbunga chenge yataendelea kusababisha vipindi vichache vya mvua kwa usiku wa tarehe 27 Oktoba 2025 na siku ya 28 Oktoba 2025, hususan katika maeneo ya pwani.
Hata hivyo, mamlaka hiyo imebainisha kuwa hakuna madhara makubwa yanayotarajiwa kutokana na hali hiyo.
“Tunaendelea kufuatilia mwenendo wa mabaki ya kimbunga chenge na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa nchini. Tutaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.”
Kwa upande mwingine, watumiaji wa bahari na wananchi kwa ujumla wametakiwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa.
"Watumiaji wa bahari na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta."
Tags
CHENGE Cyclone
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania