Machifu wa Mikoa ya Kusini wana jambo lao Mbeya

MBEYA-Shirika la Akida Wabu Development Foundation (AWADEF) kwa kushirikiana na Umoja wa Machifu wa Mikoa ya Kusini na Serikali wanatarajia kuendesha semina kubwa ya siku nne kwa ajili ya kuwajengea uwezo Machifu kutoka mikoa tisa ya Kusini mwa Tanzania.
Semina hiyo itakayofanyika kuanzia Oktoba 9 hadi 12, 2025 jijini Mbeya, inatarajiwa kukutanisha zaidi ya washiriki 220, wakiwemo Machifu kutoka mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Njombe, Iringa, Songwe, Mbeya, Morogoro pamoja na taasisi mbalimbali za serikali na binafsi.

Chifu Saad Wabu Mussa Mitondo II, Mwenyekiti wa Akida Wabu Development Foundation ambaye pia ni Katibu wa Machifu Mkoa wa Ruvuma na Chifu Kapere Said Kapere, Kaimu Katibu wa Umoja wa Machifu Mikoa ya Kusini wameyasema hayo leo Oktoba 4,2025 jijini Mbeya wakati wakizungumza na waandishi wa habari.

Wamebainisha kuwa,lengo kuu la semina hiyo ni kuwawezesha Machifu kufahamu masuala muhimu ya uongozi wa kisasa ikiwemo itifaki, ulinzi wa mtoto, sayansi ya malezi, mifuko ya uwekezaji, bima ya afya na uzalendo.
Mada hizo zitatolewa na wataalamu kutoka mashirika kama UNICEF, TECDEN, NEMC, UCSAF, NHIF, WCF, Mahakama ya Tanzania na wengine.

“Kaulimbiu yetu kwa semina hii ni ‘Uongozi wa Kimila kwa Amani, Uwajibikaji, na Maendeleo Endelevu."

Kwa mujibu wa viongozi hao, mgeni rasmi anayetegemewa kufungua semina ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, huku Mhe. Dkt. Pindi Hazara Chana, Waziri wa Maliasili na Utalii, akitarajiwa kuwa mgeni maalum.

Pia, Mhe. Ridhiwani Kikwete, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu, anatarajiwa kutoa mada kuhusu historia ya Machifu Tanzania.

Semina hii inakuja wakati ambapo taifa linaelekea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, hivyo Machifu wanachukua jukumu la kuhakikisha kuwa amani inalindwa kwa gharama yoyote.
Mbali na semina, Matembezi ya Amani ya Mshikamano wa Machifu yanatarajiwa kufanyika Oktoba 13, 2025 jijini Mbeya, yakiongozwa na viongozi wa kimila pamoja na viongozi wa kitaifa.

Mhe. Antony Mavunde, Waziri wa Madini, na Waziri Mkuu Mstaafu, Dkt.John Samweli Malecela, wanatarajiwa kuwa miongoni mwa wageni mashuhuri kwenye tukio hilo, sambamba na Mhe.Dkt.Tulia Ackson, Spika wa Bunge.

Katika tukio hilo, GeorDavie, Nabii Mkuu wa GeorDavie Ministries, atashiriki kama Balozi wa Amani, akiongoza maombi maalum ya kuiombea Tanzania kuelekea uchaguzi mkuu.

AWADEF pia imewataka wananchi wa Mkoa wa Mbeya kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru tarehe 14 Oktoba, 2025 katika Uwanja wa Samora, ambako Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Aidha, Machifu wamewasilisha ombi rasmi kwa Rais Dkt.Samia kuwa mgeni rasmi wa kufunga semina hiyo ya kihistoria, pamoja na kukutana nao ana kwa ana katika tukio hilo.

Katika hotuba yao, Machifu wamesisitiza umuhimu wa viongozi wa kimila katika kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa.

Pia, wametajwa kama wapatanishi, walinzi wa maadili, wahifadhi wa urithi wa kitamaduni na viongozi wa mabadiliko kwenye jamii.

“Sisi hatuna nchi nyingine ya kukimbilia, tunayo Tanzania moja tu,"wamesisitiza.

Machifu wameeleza kuwa,wapo tayari kushirikiana na serikali, mashirika ya maendeleo na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa jamii zao zinapiga hatua katika nyanja zote za maendeleo.

Aidha,watoa shukrani kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa heshima kubwa anayowapa Machifu, pamoja na viongozi wengine wa serikali, wakiwemo mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kwa ushirikiano wao katika maandalizi ya semina na matembezi ya amani.

Kuhusu AWADEF

Akida Wabu Development Foundation (AWADEF) ni shirika lisilo la kiserikali lililoanzishwa kwa ajili ya kuendeleza urithi wa utamaduni wa Mtanzania na Mwafrika, pia kushirikiana na serikali katika kusukuma gurudumu la maendeleo katika nyanja za kijamii, kiuchumi, elimu, afya na maendeleo endelevu.
Shirika hili ofisi zake zipo mkoani Ruvuma, Wilaya ya Nyasa. Dhamira yao ni  kulinda na kusherehekea urithi wa kitamaduni wa Tanzania huku wakihimiza amani, umoja, elimu, uhifadhi wa mazingira na uwezeshaji wa jamii kiuchumi.

AWADEF imejitolea kuunga mkono juhudi za serikali kushughulikia changamoto kuu za kiuchumi, kijamii, kitamaduni, kuhakikisha maendeleo jumuishi na endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Pia inao umoja wa Machifu wa Mikoa ya Kusini ambao unaundwa na Machifu wanaotoka kwenye mikoa tajwa hapo awali.

Umoja huu wa Machifu kwa sasa unaratibiwa na Sekretarieti ya AWADEF kwa kipindi hiki ambapo wanajiandaa kuwa na uongozi imara katika jitihada za kuwaunganisha Machifu wote wa Mikoa ya Kusini, umoja huu una wanachama wake ambao ni Machifu kutoka mikoa ya kusini pamoja na himaya zao.

Mikoa ya kusini ina takribani Machifu wapatao 200 ambapo kama Umoja wa Machifu wanajikita kikamilifu katika kufanya kazi kwa pamoja na serikali, mashirika ya kimataifa kuendeleza urithi wa utamaduni wa mtanzania, mila, desturi pamoja na kukemea maovu katika jamii ya watanzania.

Umoja wa Machifu Mikoa ya Kusini unatarajiwa kuzinduliwa rasmi hivi karibuni taratibu zitakapokamilika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news