ARUSHA-Wiki ya mafunzo yenye lengo la kuimarisha usalama wa mionzi katika maeneo ya ukaguzi wa mizigo imehitimishwa kwa mafanikio makubwa jijini Arusha.
Mafunzo hayo, yaliyoandaliwa na Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), yalifanyika kuanzia tarehe 6 hadi 10 Oktoba 2025, yakihusisha wataalamu wanaotumia vifaa vya ukaguzi wa mizigo (Baggage Scanners) kutoka taasisi mbalimbali nchini.
Jumla ya washiriki 31 walihudhuria mafunzo hayo, wakiwemo 28 kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), mmoja kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mmoja kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), na mmoja kutoka kampuni ya usambazaji wa vifaa vya ukaguzi wa mizigo.
Mafunzo yalitolewa kwa njia ya mihadhara ya kitaalamu, majadiliano ya kina, na mafunzo kwa vitendo katika mazingira halisi ya kazi.
Akifunga rasmi mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Prof. Najat Kassim Mohammed, Mtaalamu wa TAEC Dkt. Jerome Mwimanzi amewataka washiriki kuendeleza ushiriki wao katika mafunzo ya aina hiyo mara kwa mara ili kuongeza maarifa, kuimarisha ufanisi kazini, na kuhakikisha ufuatiliaji wa sheria, kanuni na taratibu za usalama wa mionzi katika maeneo yao ya kazi.
Katika kipindi chote cha mafunzo, washiriki walipata ujuzi na maarifa katika mada muhimu zikiwemo: Utangulizi wa Mionzi Ionizing (Introduction to Ionizing Radiation), Viwango na Vitengo vya Mionzi (Radiation Quantities and Units), Matumizi ya Teknolojia za Nyuklia (Application of Nuclear Technologies), Athari za Kibayolojia za Mionzi Ionizing (Biological Effects of Ionizing Radiation),Kanuni za Ulinzi dhidi ya Mionzi (Principles of Radiation Protection), Mfumo wa Kisheria wa Udhibiti wa Mionzi Tanzania (Regulatory Framework in United Republic of Tanzania), Majukumu ya Maafisa wa Usalama wa Mionzi (Responsibilities of Radiation Safety Officers), Ulinzi wa Wafanyakazi dhidi ya Mionzi (Radiation Protection of Workers),
Mahitaji ya Usalama wa Mionzi katika Matumizi ya Mashine za Ukaguzi wa Mizigo (Radiation Safety Requirements in the Use of Cargo Scanners), Utangulizi wa Ubora wa Picha na Utambuzi (Introduction to Image Quality and Identification),
Utangulizi wa Vifaa vya Kugundua Mionzi (Introduction to Radiation Detection Equipment), Kanuni za Msingi katika Matengenezo na Urekebishaji wa Vifaa vya Mionzi (Basic Principles in Maintenance and Repair of Radiation Devices and Detectors),
Muhtasari wa Vifaa vya Ufuatiliaji wa Mionzi katika Njia za Kupitia (Overview of Radiation Portal Monitors), Usalama wa Nyuklia na Biashara Haramu ya Vifaa vya Mionzi (Nuclear Security and Illicit Trafficking), na Muhtasari wa Ajali za Mionzi (Overview of Radiological Accidents).
Washiriki walieleza kufurahishwa na mafunzo hayo, wakisema yamewapa maarifa mapya na kuimarisha uwezo wao wa kulinda usalama wa abiria na mizigo katika maeneo ya bandari, viwanja vya ndege na vituo vya ukaguzi.
“Sasa tunaelewa si tu jinsi ya kuendesha mashine, bali pia namna ya kujilinda na kuwalinda wengine dhidi ya madhara ya mionzi,” alisema mmoja wa washiriki kutoka TPA.
Kwa TAEC, mafanikio ya mafunzo haya ni sehemu ya mkakati mpana wa kuhakikisha matumizi salama ya mionzi nchini na kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia kwa maendeleo endelevu ya taifa.











