Maji ya miji 28 sasa kuibadili Rujewa

RUJEWA-Kila kukicha na jua kuchomoza ni mwanzo wa pilikapilika mpya kwa maisha ya Mtanzania na mwanadamu yoyote duniani katika mahitaji ya kila siku ili kujiletea maendeleo na kujipatia mahitaji muhimu.
Kazi ikiendelea katika mradi wa maji wa miji 28 mjini Rujewa ikiwa ni sehemu ya ujenzi wa tanki la kuhifadhi maji kabla ya kuwafikia wateja.

Simulizi hii haina tofauti na wakazi wa eneo la Rujewa mkoani Mbeya, ambapo kila asubuhi huanza kwa pilikapilika za kina mama na watoto kusaka huduma ya maji. 

Serikali kwa kuona hilo, imeamua kuwekeza fedha ili nguvu hiyo sasa ielekezwe katika maeneo mengine, ni kuibuka matumaini mapya kwa wananchi hao.

Ni kupitia Mradi wa Maji wa Miji 28, unaotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa uongozi na sapoti kubwa kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ajenda kuu anayoisimamia kwa muda sasa ni “kumtua mama ndoo ya maji kichwani”, faraja kubwa inawajia wakazi wa Rujewa,

Mradi wa maji wa miji 28 Rujewa ni majibu ya kilio cha muda kilichoitikiwa na Serikali, ndivyo kwa maana ya kuhakikisha wananchi katika kila kona ya nchi wanapata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza. Hivyo, hatua hii inaondosha uhaba wa huduma ya uhakika ya maji safi na salama katika eneo hilo.

Ni takribani zaidi ya miaka 45, wakazi wa maeneo mradi unapotekelezwa walitegemea miundombinu ya huduma ya maji ya kale miaka ya sabini ambayo haikukidhi mahitaji kwa idadi ya watu, na mji kukua kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi, hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya sasa. 

Mradi huu mpya unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi 189,685 wa Rujewa.Ni matunda ya diplomasia na ziara ya Rais Dkt. Samia katika nchi washirika wa maendeleo ambao ni marafiki wakubwa wa nchi ya Tanzania katika kuwaletea wananchi maendeleo.

‘Akufaaye kwa dhiki, ndiye rafiki’, hivyo mradi huu unafadhiliwa kwa mkopo nafuu kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim (India), kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 20.37.

Utekelezaji wa mradi hadi sasa, zaidi ya Dola za Marekani milioni tano zimeshatumika, ikiwa ni utekelezaji wa asilimia 28.5 ya mradi na kazi inaendelea.

Mradi unatumia chanzo kikuu cha maji cha Mto Mbarali, ambapo uzalishaji wa maji uliopimwa ni lita milioni 40 kwa siku. Kati ya lita hizo milioni 40; Rujewa itapata lita milioni 15, miji ya Makambako na Wanging’ombe ikinufaika na lita milioni 25 kwa pamoja. Hatua iliyochukuliwa na Serikali itaondosha uhaba wa huduma ya maji kwa miundombinu ya kisasa, kuongeza tija katika sekta mbalimbali ikiwamo za afya, elimu na uchumi.

Utekelezaji wa mradi ulianza rasmi tarehe 11 Aprili 2023 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2025. Hivi sasa kazi zinazondelea ni pamoja na ujenzi wa mtambo wa kutibu maji, ulazaji wa mabomba makuu, na ujenzi wa matenki ya kuhifadhia maji.

Mafanikio makubwa ya mradi huu yanatokana pia na ushirikishwaji wa wananchi. Kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali za Mitaa, baadhi ya wananchi kujitolea ardhi na nguvu kazi kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu hivyo ushirikiano huu kurahisisha utekelezaji wa mradi kwa kiasi kubwa.

Mradi unatekelezwa na wakandarasi Kampuni ya Larsen & Toubro Construction kutoka India, na kusimamiwa na kampuni ya WAPCOS Ltd ya India kwa ushirikiano na kampuni za GSB, Upimark, na Mhandisi Consultancy kama Wahandsi Washaur.

Wakazi wa eneo mradi unapotekelezwa wanayo mengi ya kusema. Kwa uchache Bi. Aurelia Kayombo, mkazi wa Kitongoji cha Kamficheni, Kata ya Lugelele, Rujewa, amesema kumekuwa na changamoto kwa wanafunzi kubeba maji kutoka nyumbani na kutumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kusoma.

“Tuliposikia kuhusu mradi huu tulifurahi sana kwa sababu bila shaka ni suluhisho kwa changamoto nyingi, hasa sisi wanawake,watoto wetu pamoja na familia kwa ujumla” Aurelia ameeleza.

Kauli hii inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Kijiji cha Igomelo, Bw.Nickson Ngela, ambaye amesema kuwa mfumo wa sasa ulijengwa kwa ajili ya wakazi 330 pekee mwaka 1979, hivyo kwasasa hautoshelezi. “Tuna matumaini makubwa na mradi huu mpya kukidhi mahitaji. Ukikamilika, utabadilisha kabisa maisha yetu ya kila siku,” Ngela amesema.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mbarali Dkt. Jackson Njugilo, amesema hospitali ya Mbarali hupata maji kwa mgao, kwa maana ya mara tatu kwa wiki, hivyo kutotosheleza kwa mahitaji ya huduma mbalimbali katika hospitali hiyo.

“Huduma ya maji ya uhakika itapunguza magonjwa ya mlipuko katika jamii na kuongeza ufanisi wa huduma za afya kwa wakazi 45,354 wanaohudumiwa na hospitali yetu,” Dkt. Njugilo amebainisha na kuongeza gharama zinazotumika zitashuka na nguvu kazi itatumika kuinua uchumi badala ya muda mwingi kutumika katika matibabu.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Rujewa (RUJEWASA), Mhandisi Restus Linda amesema kuwa mradi unajumuisha ujenzi wa banio la maji litakalozalisha lita milioni 41 kwa siku, pamoja na mtambo wa kisasa wa kutibu maji wenye uwezo wa kusafisha maji lita milioni 40 kwa siku.

Pia, kunajengwa majengo ya ofisi, nyumba za watumishi, maabara ya maji, nyumba za walinzi na uzio kwa ajili ya usalama wa miundombinu hiyo.

Hadi sasa, usanifu wa banio, ulazaji wa mabomba makuu, na bomba za usambazaji maji umekamilika.

Aidha, maeneo yote yatakayopitiwa na miundombinu yameshatambuliwa na alama muhimu kuwekwa. Walioathiriwa na ujenzi wa mradi tiyari wameshalipwa fidia.

Ujenzi wa mtambo unaendelea pamoja na ujenzi wa majengo muhimu kama jengo la kutunzia dawa za kutibu maji kabla ya kufika kwa wananchi.

Wananchi wa Rujewa na maeneo ya jirani wanatarajia kupata huduma ya maji kwa saa 24, huduma ambayo kwao imekuwa kama ndoto.

Mradi huu ni sehemu ya juhudi za Serikali kkatika kufanikisha mpango wa kufikisha huduma ya maji kwa wananchi kwa asilimia 95 ya wakazi wa miji na vijijini 85 kuwa wanapata huduma ya maji safi na salama. Kwa wakazi wa Rujewa, huu ni mwanzo mpya wa maisha bora, afya na maendeleo endelevu.

Hafla ya utiaji saini wa Mikataba ya Mradi wa Maji wa Miji 28 ulishuhudiwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ikulu Chamwino Jijini Dodoma tarehe 06 Juni, 2022.

Thamani ya mradi huu ambao ni moja ya miradi mikubwa kabisa ya majisafi ni Dola za Marekani milioni 500 sawa na zaidi ya shilingi Trilioni moja ikiwa ni mkopo wa masharti nafuu kutoka serikali ya India kupitia Benki ya Exim India.

Mradi wa Maji wa Miji 28 utanufaisha miji ya Kaliuwa, Sikonge, Urambo, Kasulu, Mpanda,Kilwa Masoko, Nanyumbu, Ifakara, Rujewa, Makambako, Njombe, Wangingombe, Chunya,Chamwino, Chemba, Singida, Manyoni, Mugumu, Geita, Kayanga, Chato, Handeni, Korogwe, Muheza, Pangani, Mafinga, Songea, Rorya / Tarime, na Makonde.

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akitembelea maonesho wakati wa Wiki ya Mazingira jijini Dodoma, hivi karibuni, amesisitiza pamoja na kazi kubwa inayofanywa na Serikali, suala la wananchi na wanufaika wengine kushirikishwa katika kulinda mazingira ni muhimu.

Wanazuoni katika tafiti mbalimbali wanasema kwa uchache utunzaji mahiri wa mazingira na vyanzo vya maji, ni muhimu kwa maisha ya kila kiumbe hai na vinginevyo maisha yatakuwa hatarini. Hii ni kwa sababu mazingira salama ndiyo chanzo cha uhai kwa viumbe vyote.

Ni dhahiri kuwa maisha yanategemea sana maji, mimea na hewa ili kuishi. Vivyo hivyo maisha ya mimea yanategemea maji na hewa katika uhai wake, ni sayansi rahisi kabisa kuelewa.

Sio katika nchi za ulimwengu wa tatu pekee, hata mataifa yaliyoendela, tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa mijini na vijijini, limekuwa ni kero kubwa na limechangiwa pakubwa kwa uharibifu wa vyanzo vya maji na mfumo wa maji , pamoja na changamoto za mazingira zinazoendelea kuikabili dunia, ingawa jitihada mbalimbali katika kukabiliana na changamoto hizo zinachukuliwa.

Kwa maana fupi mazingira ni jumla ya vitu vyote vinavyo mzunguka kiumbe hai katika maisha yake kama hewa, maji na mmea. Ili kiumbe hai aweze kuishi vizuri anahitaji mazingira safi na salama. Kwa kawaida mazingira yanahitaji utunzaji wa hali ya juu ili yaweze kuwa safi na salama.

Kwa mantiki hiyo basi maisha ya viumbe hai wa kizazi kilichopo na kijacho kinategemea uwepo wa mahusiano mazuri ya utunzaji wa mazingira

Utunzaji wa mazingira ni hali au kitendo cha kuyaweka mazingira katika hali ya usafi na salama ili kudumisha maisha ya viumbe hai. Maisha ya viumbe hai yanahitaji uwepo wa mazingira safi na salama.

Asilimia kubwa ya mazingira duniani kama vile vyanzo vya maji, hali ya hewa vinazidi kuchafuliwa kwa sababu mbalimbali.

Utunzaji wa mazingira ni sehemu muhimu katika maendeleo ya kila siku ya mwanadamu kama ilivyo muhimu damu kwa maisha ya viumbe hai ,Watalamu wa masula ya mazingira husema bila maji hakuna maisha na ili maji yapatikane lazima vyanzo hivyo vya maji vilindwe, “maji ni uhai”.

Uharibifu wa mazingira ni pamoja na uzoroteshaji wa mazingira kwa njia ya kupunguza rasilimali ikiwamo maji. Uharibifu wa mazingira ni wa aina nyingi. Maliasili kutumiwa vibaya, ni uharibifu wa mazingira.

Ukataji wa misitu, uchafuzi wa mazingira baharini na nchi kavu, uchafuzi wa maji na hali ya hewa ni baadhi ya mambo yanayotishia kuangamiza mazingira asilia duniani.

Uharibifu wa mazingira ni moja ya vitisho kumi vilivyoonywa na jopo la juu la vitisho vikuu kutoka Umoja wa Mataifa (UN).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news