DODOMA-Jeshi la Polisi Tanzania limekanusha taarifa zinazosambazwa kupitia vyombo vya habari zikidai kuwa watu saba wamekamatwa katika mazingira ya kutatanisha, likisema kuwa waliokamatwa walitiwa nguvuni kwa mujibu wa sheria kutokana na tuhuma za uhalifu, zikiwemo za uchochezi na kuhamasisha maandamano yasiyo halali.
Kupitia taarifa yake kwa umma iliyotolewa Oktoba 17, 2025, Makao Makuu ya Polisi Dodoma, kupitia Msemaji wake DCP David Misime, jeshi hilo limesema,miongoni mwa watu sita waliotajwa katika taarifa hizo, walikamatwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
Ni kutokana na ushahidi uliokuwa umekusanywa kabla ya kukamatwa kuhusiana na tuhuma mbalimbali za kihalifu.
Jeshi hilo limefafanua kuwa,watuhumiwa hao walikamatwa kwa kosa la matumizi mabaya ya mitandao kwa kufanya uchochezi na kuhamasisha maandamano kinyume cha sheria.
"Wakati wa ukamataji watu walishuhudia na baadhi ya viongozi wao walifika katika ofisi za makamanda wa polisi mikoa na vituo vya polisi kuwaulizia, na walijulishwa kuwa watu sita wanashikiliwa na walielezwa tuhuma zao," taarifa hiyo imeeleza.
Jeshi la Polisi limewataja waliokamatwa kuwa ni Chief Adronius Kalumuna, Paulo Shijason Musisi, Daniel Damian Lwebugisa, Egbert Aloyce Kikulega, Ramadhan Fadhiri na Baziri Waziri.
