DAR-Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Chumi, amekutan na kuzungumza na Balozi wa Cuba nchini, Mhe. Yordenis Despaigne Vera, katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar Es Salaam. 

Mazungumzo hayo yalilenga kujadili namna ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Cuba.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Chumi amesisitiza umuhimu wa Serikali za Tanzania na Cuba kuweka mikakati madhubuti ya kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia.
Ameishukuru Serikali ya Cuba kwa kuendelea kushirikiana karibu na Tanzania hasa katika sekta ya afya, elimu, viwanda na diplomasia.
“Tanzania imenufaika na madaktari wa kujitolea kutoka Cuba, fursa za masomo kwa wanafunzi katika taaluma za afya na sayansi, pamoja na uanzishaji wa kiwanda cha viuatilifu Kibaha mkoani Pwani, na msaada katika sekta ya kilimo.
"Kimsingi, mataifa haya yameimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kutetea haki za nchi zinazoendelea na kusisitiza mshikamano wa kimataifa,"alifafanua Mhe.Chumi.
Naye Balozi wa Cuba nchini Mhe. Yordenis Vera ameishukuru Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano na nchi yake, na emeelezea umuhimu wa kukuza ushirikiano katika diplomasia ya Uchumi husuani katika sekta za biashara, viwanda, teknolojia, utamaduni na michezo.












